Yanga yafunguka ilivyoizidi Simba kumtuliza Tshishimbi

24Mar 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yafunguka ilivyoizidi Simba kumtuliza Tshishimbi

BAADA ya kufanikiwa kumshawishi kiungo wake wa kimataifa Papy Tshishimbi kubakia klabuni kwake, uongozi wa Yanga umesema ulifahamu mipango waliyokuwa nayo wapinzani wao, Simba katika kumwinda Mkongomani huyo, imeelezwa.

Tayari Yanga na Tshishimbi wamefikia katika hatua nzuri ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao inakaribia kumalizika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema wamefikia katika hatua nzuri na kiungo huyo ambaye ni mmoja wa wachezaji ambao wamependekezwa na Kocha Luc Eymeal kubakia klabuni hapo.

Mwakalebela alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo utaendelea na mchakato wa kuwapa mikataba mipya nyota wote ambao wameonyesha kiwango kizuri na benchi la ufundi linahitaji kuendelea kufanya nao kazi katika msimu ujao.

"Baada ya kufanikisha kwa Bernard Morrison, sasa tunaendelea na mchakato wetu wa kuzungumza na wachezaji wengine ambao mikataba yao ipo ukingoni, tayari tumeshakutana na Tshishimbi kwa ajili kumwongezea mkataba mpya wa kuitumikia timu yetu," alisema Mwakalebela.

Aliongeza kuwa wanaamini usajili watakaofanya sasa utalenga kutimiza mipango ya kufanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano yote watakayoshiriki ndani na nje ya nchi.

"Tunachokifanya ni kuendelea kukijenga kikosi chetu, tunataka kuwa na timu bora zaidi ya sasa, timu itakayokuwa inatupa matokeo chanya katika kila mechi, Mwakalebela alisema.

Aliongeza kikosi chao kimekuwa na mabadiliko tangu ujio wa Mbelgiji Eymael na wanaamini kitaendelea kuwa imara na kufanya vema katika michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Bara na mashindano ya Kombe la FA.

Habari Kubwa