Yanga yahofia hujuma ugenini

10Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
Yanga yahofia hujuma ugenini

YANGA imeaondoka leo alfajiri kwenda Mauritius kwa ajili ya mchezo wao wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim Jumamosi wiki hii, huku ikijiami vilivyo na uwezekano wowote wa kufanyiwa hujuma.

Yanga inashuka dimbani mwishoni mwa wiki hii kucheza mechi ya kwanza ya michuano hiyo yenye hadhi kubwa katika ngazi ya klabu.

Katika kukwepa hujuma, klabu hiyo haitafikia hotelini, badala yake wataweka kambi katika eneo ambalo halikutajwa, lakini likiwa na huduma zote muhimu.

Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema dhamira yao ni kushinda mchezo huo, lakini pia wanajiandaa kukabiliana na hujum zozote.
"Unajua katika mechi kubwa kama hizi kuna mambo mengi, hujuma nazo hazikosekani," alisema Muro.

"Tumepata eneo itakapofikia timu, tutafanya mazoezi hapo na kila kitu tutamaliza hapo kabla ya kwenda kwenye mchezo."

Kuhusu wachezaji wanaosafiri, Muro alisema Kocha, Hans van der Pluijm, amemjumuisha nahodha, Nadir Haroub 'Canavaro' baada ya ripoti ya daktari kuonyesha amepata nafuu.

Pia wachezaji Haji Mwinyi na Thaban Kamusoko waliokuwa majeruhi, wamejumuishwa kwenye safari hiyo itakayokuwa na wachezaji 21 na viongozi saba.

Aidha, Geofrey Mwashiuya, Benedicto Tinnoco na Matheo Simion hawataongozana na timu.

"Tinnoco na Mwashiuya wana matatizo kwenye hati zao za kusafiria, lakini Matheo yeye anaachwa kwa kuwa hayupo fiti kwa ajili ya mchezo huu," aliongezea kusema Murro.

Akizungumzia mechi hiyo, Pluijm alisema atakiongoza kikosi chake kushambulia mwanzo mwisho wa mchezo.

Alisema hawatacheza mchezo wa kujiami kwa vile watakuwa ugenini, badala yake watashambulia mfululizo ili kupata ushindi kwenye mechi hiyo.

"Tunaenda kupambana, hakuna mechi ndogo wala nchi ndogo katika ulimwengu huu wa soka. Tutacheza kwa kushambulia na siyo tu kulinda lango letu na kusahau kutafuta mabao," alisema Pluijm.
"Msimu huu tunataka kuweka rekodi mpya kwenye michuano ya kimataifa. Naamini kikosi changu kinaweza kuandika historia hiyo."

Pluijm alisema kwamba mechi mbili za ugenini za Ligi Kuu Bara walizocheza wiki iliyopita na kuambulia pointi moja zimewasaidia kuwaamsha upya wachezaji wake.
Msafara wa Yanga utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayoub Nyenzi.

Habari Kubwa