Yanga yaiandalia dozi KMC

10Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaiandalia dozi KMC
  • ***Lengo ni kujiimarisha katika mbio za ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara na...

JESHI la Yanga linatarajia kuendelea na mbio za kuwania ubingwa kwa kuwakaribisha 'Watoto wa Kinondoni' KMC FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Hata hivyo katika mechi yake ya mwisho, vinara hao wa Ligi Kuu Bara walilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya 'Maafande' wa Polisi Tanzania ambao makao makuu yao yako Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi alisema kikosi chao kipo fiti na tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao wanafahamu utakuwa na ushindani.

Mwambusi alisema kikosi chake kimejipanga kucheza soka la kushambulia ili kuhakikisha wanashinda na kujiimarisha katika nafasi waliyopo kwenye uongozi wa ligi hiyo ya juu Tanzania Bara.

"Kila mechi kwetu ni fainali, tumejipanga vizuri, na wachezaji wote wako fiti kasoro watatu ambao hawako katika mipango yetu ya mchezo huo, ni habari nzuri kwetu kwa mshambuliaji wetu, Saido Ntibazonkiza amerejea na atakuwa miongoni mwa nyota watakaoanza,".

"Carlos Carlihnos yuko fiti ila hatokuwapo kwenye kikosi  kitakachoanza lakini pia tutawakosa Farid Mussa, Yassin Mustapha ambao wanasumbuliwa na malaria, lakini Haruna Niyonzima hayuko kwenye mipango ya mchezo huo kwa sababu ameingia kambini jana (juzi) akitokea kwenye majukumu ya timu ya Taifa," alisema Mwambusi.

Nahodha wa Yanga, Lamine Moro alisema wamejipanga vizuri kwa ajili ya kupambana na kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu muhimu katika mchezo huo na kuzikimbia timu zinazowafuata.

"Tunasikia maneno mengi nje ya uwanja ila sisi hatujali, tumejiandaa kwenda uwanjani kupambana ili kutafuta matokeo mazuri kwenye mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa," alisema Moro.

Habibu Kondo, Kaimu Kocha Mkuu wa KMC FC, alisema wachezaji wake hawatakuwa tayari kupoteza mara mbili mechi dhidi ya Yanga katika msimu mmoja.

"Tumejipanga vizuri, tunawaheshimu wapinzani wetu, wana kikosi kizuri ila hatutaogopa kwa kuwa wanaongoza ligi, kwa sababu tumejiandaa kutafuta matokeo chanya katika mchezo huo," alisema Kondo.

Naye nahodha wa KMC FC, Juma Kaseja, alisema kazi iliyobaki ni kwao kutekeleza maelekezo waliyopewa baada ya kocha na benchi la ufundi kumaliza majukumu yao ya kuwafundisha na kuwapa mbinu za kwenda kutafuta ushindi katika mchezo huo.

"Hautakuwa mchezo rahisi, kwa sababu tumejipanga vizuri na kocha amemaliza majukumu yake, sasa kazi kubwa imebaki kwetu kuhakikisha tunapambana kutafuta matokeo chanya," alisema Kaseja.

Yanga yenye pointi 50 ndio vinara wa ligi hiyo wakifuatiwa na watani zao na mabingwa watetezi Simba wenye pointi 46, lakini wamecheza mechi tatu pungufu.

Habari Kubwa