Yanga yaigaragaza Simba usajili nyota

04Jun 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Yanga yaigaragaza Simba usajili nyota
  • ***Yanasa wakali waliokuwa wakiwaniwa Msimbazi, akiwamo Mayanga na...

KATIKA kuimarisha kikosi chake ili kiweze kurejesha makali yake msimu ujao, Yanga imewazidi kete watani zao mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kwa kumsajili mshambuliaji kutoka Ndanda FC ya Mtwara, Vitalis Mayanga na golikipa, Farouk Shigalo kutoka Bandari ya Kenya.

Farouk Shigalo kutoka Bandari ya Kenya.

Simba ilikuwa katika rada za kutaka kumsajili Mayanga baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mzunguko wa kwanza wa msimu uliomalizika, lakini kabla ya kukamilisha mchakato huo, tayari Yanga yenye uongozi mpya, imefanikiwa kunasa saini ya mshambuliaji huyo.

Taarifa kutoka Yanga, zinaeleza kuwa imemsajili mshambuliaji huyo kwa kumpa mkataba wa miaka miwili baada ya kukamilisha mazungumzo na nyota huyo kuridhia kujiunga na klabu hiyo inayofundishwa na Kocha Mwinyi Zahera kutoka DR Congo.

Habari zaidi zinaeleza kuwa Yanga imeendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwa kumsajili Shigalo, ambaye alikuwa anaichezea klabu hiyo ya Ligi Kuu Kenya pamoja na Timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars) kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.

Kiongozi mmoja wa klabu hiyo (jina tunalihifadhi), aliliambia gazeti hili jana kuwa klabu yake imewasajili Mayanga ambaye alikuwa amemaliza mkataba na Ndanda pamoja na Shigalo kama ambavyo kocha wao, Zahera alivyopendekeza katika ripoti yake.

"Ndio, tumemsajili kama mchezaji huru, mkataba wake na Ndanda FC umeshamalizika, sasa rasmi Mayanga ni mchezaji wa Yanga, amesaini miaka miwili," alisema kwa kifupi kiongozi huyo.

Yanga ilianza kumfuatilia mshambuliaji huyo katika kipindi cha dirisha dogo mwaka jana, lakini mchakato wa kumsajili ulishindwa kukamilika kirahisi kutokana na nyota huyo kubanwa na mkataba wake.

Msimu uliomalizika Yanga imemaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Simba, huku pia ikipoteza tiketi nyingine ya kushiriki mashindano ya kimataifa baada ya kukubali kutolewa katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA na Lipuli ya Iringa.

Hata hivyo, bado Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halijafungua rasmi dirisha la usajili wa wachezaji kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Habari Kubwa