Yanga yaipatia ahueni Simba

09Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Yanga yaipatia ahueni Simba
  • ***Mashabiki walia, wafurahia na kushukuru kutolewa Mapinduzi Cup...

NI furaha na huzuni! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema pindi unapochukua hatua kuelezea hali halisi ilivyokuwa kwenye Uwanja wa Amaan juzi usiku, wakati Yanga ikipoteza matumaini ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Katika mechi hiyo, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Malindi ambayo imejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza nusu fainali.

Matokeo hayo yanaifanya Malindi kufikisha alama saba sawa na Azam FC iliyopo kileleni mwa Kundi B, huku Jamhuri ikishika nafasi ya nne kwa pointi zake nne na Yanga ikibaki nafasi ya nne na alama tatu wakati KVZ ikiburuza mkia kwa pointi moja.

Hata hivyo, matokeo hayo ya Yanga yalipokelewa kwa hisia tofauti kufuatia baadhi ya mashabiki wake kuyafurahia na kuhisi ahueni kwa kuiepuka Simba na wengine wakiangua kilio.

Baadhi ya mashabiki walioangua kilio ni wale waliokerwa na kipigo na matokeo ya timu yao kwa ujumla, huku waliofurahia wakiwa ni wale walishukuru kutolewa kwa kuwa imeepuka kukutana na "moto" wa watani zao, Simba endapo Yanga ingetinga nusu fainali kwa kumaliza nafasi ya pili katika Kundi B, ingekutana na Simba ambayo jana ilikuwa na nafasi kubwa ya kumaliza kileleni mwa Kundi A itakapokutana na Mlandege.

"Hii ni aibu kubwa sana, kwenye soka kila kitu kinabaki kuwa rekodi, hii haiwezi kufutika kwamba tarehe ya leo (Januari 7, 2019) Malindi wameifunga Yanga.

"Sijui kwa nini viongozi wetu wanakuwa waoga wa mashindano, tunabaki wakati timu tunayo? Hata siku moja kwenye rekodi haiwezi kuandikwa Malindi ilikifunga kikosi cha pili, jina linabaki kuwa Yanga tu," alisema Abdallah Musa aliyejitambulisha kuwa shabiki wa Yanga.

Naye Masauni Yusuf huku akibubujikwa na machozi, alisema ni fedheha na aibu na ingawa inauma, lakini anashukuru Yanga kutolewa.

"Mimi ni shabiki kindakindaki wa Yanga, lakini bora tumetolewa maana ingekuwa aibu kukutana na Simba tupigwe thalatha ama mkono.

"Ingebaki kuwa rekodi na hata kama hii ni timu B, unafikiri huu muziki wa Simba ni ngoma ya kitoto? Hata Yanga wakubwa lazima tujipange, bora tumetolewa japo inauma," alisema Yusuf.

Akizungumzia matokeo hayo, Meneja wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro', alisema anakipongeza kikosi chao kwa uwezo kilioonyesha na anaamini kimepata mazoezi mazuri.

Habari Kubwa