Yanga yaitafutia pumzi Alliance

20Mar 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaitafutia pumzi Alliance

BAADA ya mapumziko ya siku tatu, kikosi cha Yanga leo kinaanza mazoezi kujiwinda na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho (FA), dhidi ya Alliance ya Mwanza.

Yanga baada ya mchezo wao dhidi ya Lipuli, wachezaji walipewa mapumziko mafupi na leo wanarejea kwenye mazoezi chini ya kocha msaidizi, Noel Mwandila.

Akizungumza na Nipashe jana, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema kuwa Yanga inatarajia kwenda Mwanza Machi 28, mwaka huu tayari kwa mchezo huo.

"Kesho (leo), tunaanza mazoezi chini ya kocha Mwandila kwa ajili ya mchezo wetu wa Kombe la FA," alisema Saleh.

Aidha, alisema kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera anatarajia kurejea nchini mara baada ya mchezo wa timu ya Taifa ya Congo dhidi ya Gabon utakaochezwa Jumapili ijayo.

"Kwenye mchezo wa Mwanza atakuwapo, lakini kwa sasa benchi la ufundi lipo chini ya kocha msaidizi," alisema.

Mchezo huo wa Kombe la FA utachezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo mshindi atasonga mbele hatua inayofuata.

Bingwa wa michuano hiyo ya FA ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Habari Kubwa