Yanga yaiteka Iringa

16Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Iringa
Nipashe
Yanga yaiteka Iringa

YANGA wameisimamisha Iringa, ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mashabiki wa soka mkoani hapo kuusubiri kwa shauku kubwa mchezo wa leo dhidi ya Lipuli FC.

Yanga wanashuka kwenye uwanja wa Samora mjini hapo kujaribu kuendeleza wimbi lao la ushindi watakapowakabili Lipuli chini ya kocha wao Seleman Matola ambaye amewatahadharisha wapinzani wao hao kutotarajia mteremko.

Matola, aliliambia gazeti hili kuwa anafahamu Yanga wana kikosi kizuri lakini kwa maandalizi aliyoyafanya kuelekea mchezo wa leo, hawatarajii kupoteza pointi.

“Tumejiandaa vizuri, tunafahamu Yanga wanakuja wakiwa na morali ya ushindi, lakini vijana wangu wamejiandaa vyema na naamini ushindi ni wetu,” alisema Matola.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, amesema matokeo yatajulikana baada ya dakika 90 za mchezo, lakini anaamini wachezaji wake wakifuata maelekezo wana nafasi ya kuondoka na pointi tatu.

“Mpira ni dakika 90… tumejiandaa kupambana kwa dakika hizo zote, matokeo yatajulikana baadaye, lakini tumekuja hapa kupambana kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu,” alisema Mwandila.

Yanga leo itaingia uwanjani bila ya nyota wake, Andrew Vincent, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Nahodha wake Ibrahimu Ajibuambaye ambao ni majeruhi wa nyonga.

Habari Kubwa