Yanga yaitisha Mbeya Kwanza

20May 2022
Saada Akida
DAR
Nipashe
Yanga yaitisha Mbeya Kwanza
  • ***Yatamba itatumia nguvu ile ile kwa sababu inahitaji ushindi na...

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanatarajia kuwakaribisha Mbeya Kwanza kutoka Mbeya katika mechi ya ligi hiyo itakayochezwa leo kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi.

Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa kesho lakini ukarudishwa nyuma siku moja kutokana na mabadiliko yaliyotolewa katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji wakati Mbeya Kwanza yenyewe ilifungwa goli 1-0 na Geita Gold, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji Mjini Songea.

Enock Jiah wa Mbeya Kwanza anatarajiwa kukosekana kwenye mchezo huo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Geita Gold.

Akizungumza jijini jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi, alisema mechi hiyo ni mechi ya kawaida lakini wanatakiwa kujiandaa zaidi kwa sababu timu zilizoko mkiani hucheza kwa kukamia pale wanapokutana na vigogo.

Nabi alisema watacheza kwa tahadhari kubwa katika mchezo huo kwa sababu hataki kurudia kile kilichotokea walipokutana na Tanzania Prisons ambapo waligawana pointi.

“Tunajua tunaenda kucheza na timu ambayo iko chini na wanahitaji kupata matokeo mazuri ili kujiweka sehemu salama dhidi ya janga la kushuka daraja, lakini upande wetu tunahitaji pointi tatu ili kujiweka imara katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hii,” alisema Nabi.

Kocha huyo alisema katika mchezo huo kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi chake kwa sababu anahitaji kutoa nafasi kwa kila mchezaji kwenye michezo iliyobakia na kusaidia timu yao.

“Suala la ubingwa bado Yanga haijakuwa bingwa, akili zote tunaumiza kichwa katika mechi zilizoko mbele yetu hasa ukizingatia ndani ya siku tisa kuna mechi tatu, lazima kuwepo na mabadiliko ya kikosi, wengine tutawapa mapumziko kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA,” Nabi alisema.

Naye Kocha Msaidizi wa Mbeya Kwanza, Aswile Asukile, alisema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanakuwa timu ya kwanza kuifanyia maajabu Yanga.

“Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Yanga iko vizuri, suala la kutokuwapo benchi kwa kocha wetu mkuu (Mbwana Makata), hatujaathirika na mipango yetu ya kutafuta pointi katika mchezo huu dhidi ya Yanga,” alisema Aswile.

Nahodha wa Mbeya City, Mohammed Kapeta, alisema: “Tumejiandaa vizuri na tunatambua Yanga iko vizuri, hawajapoteza mechi na tunaenda kupambana kutafuta pointi katika mchezo huo.”

Mbeya Kwanza inaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 21 huku timu nyingine iliyoko kwenye janga hilo la kushuka daraja ni Tanzania Prisons na Biashara United.

Mechi nyingine za ligi hiyo zitaendelea tena kesho kwa Mtibwa Sugar kuikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Morogoro wakati Ruvu Shooting itawafuata Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba.

 

Habari Kubwa