Yanga yaitiwa Chama, Fraga

11Aug 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaitiwa Chama, Fraga
  • ***Uongozi Simba watangaza dau, wachezaji hao kila mmoja akikiri bado ana mkataba wa...

WAKATI viungo wa Simba, Mzambia Claotus Chama na Mbrazil Gerson Fraga wakizidi kuhusishwa na kujiunga na wapinzani wao, Yanga, 'Wekundu wa Msimbazi' hao, wametoa kauli 'pendwa' kwa watani zao kwa kuwaita mezani kuteta ili kumalizana, imeelezwa.

Kiungo wa Simba, Mzambia Claotus Chama:PICHA NA MTANDAO

Tangu kuibuka kwa sakata la kiungo wa Yanga, Mghana Bernard Morrison kutangazwa kutia saini mkataba wa kujiunga na Simba, klabu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani nayo imekuwa ikihusishwa na kutaka kuwasajili Chama na Fraga.

Taarifa hizo zilikolezwa zaidi juzi baada ya Yanga kufanikiwa kuipata huduma ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha Mazingiza, zikidai kituo kinachofuata kwa Chama ni Jangwani kuungana na bosi huyo.

Hata hivyo, Crescentius Magori, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba na Mshauri wa Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed "Mo" Dewji, amesema watani zao hao wanaweza kuwasajili wachezaji hao kwa sasa kama tu watakubaliana dau wanalolitaka.

Magori aliliambia Nipashe jana kuwa wachezaji hao bado wana mikataba na Simba na kwamba Chama ambaye amekuwa akihusishwa zaidi na Yanga, ana uhakika huo kwa kuwa mchezaji huyo alitia saini mkataba wake mbele yake kipindi yeye akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo (CEO).

"Kama wanamtaka waje mezani, hatukatai kumuuza, endapo wana Dola 800,000 walete tutawauzia, kwani bado tuna mkataba wa mwaka mmoja naye," Magori alisema.

Nakuongeza kuwa wakati huu Chama akiwa kwao Zambia kwa mapumziko mafupi, amemueleza kuna watu wamekuwa wakimfuata wakala wake kutaka huduma yake.

Naye Ofisa Habari wa Simba, Hajji Manara alitoa ufafanuzi zaidi akisema mwaka jana, nyota huyo na wengine akiwamo Meddie Kagere waliongeza mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika Julai 2021.

"Mkataba wa awali wa Chama ulikuwa unaisha Julai 2020, mwaka jana aliongeza mwaka mmoja ambao sasa utamalizika 2021, pamoja na nyota wetu wengine wanaotajwa.

"Yanga au timu yoyote kama wanamtaka Chama na wachezaji waliokuwa na mikataba walete barua ya kuomba kumsajili, sisi hatuweza kwenda kwa Feisal Toto mwenye mkataba na kumsajili," alisema Manara.

Kwa upande wa Fraga, akizungumza na Nipashe kwa simu jana kutoka kwao Brazil alipo kwa mapumziko mafupi, alikanusha taarifa zilizozagaa kuwa ameuandikia barua uongozi wa Klabu ya Simba kuomba kuondoa kama ambavyo inadaiwa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari (si Nipashe).

Alisema bado yupo Simba na  hajamaliza mkataba, na sasa yupo kwao kwa mapumziko mafupi na atarejea mapema kabla ya muda wa kuingia kambini.

"Hizo taarifa za kuandika barua si kweli, mimi ni mchezaji halali wa Simba, mkataba wangu umebaki miezi sita, nitarudi kuitumikia timu yangu kwa msimu ujao," alisema kiungo huyo.

Simba inatarajia kuingia kambini Jumatatu ijayo kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi Namungo itakayopigwa Agosti 29 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, na kisha timu hiyo kuunganisha kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu.

Habari Kubwa