Yanga yajipanga kuimaliza Kagera

25Nov 2018
Faustine Feliciane
Kagera
Nipashe Jumapili
Yanga yajipanga kuimaliza Kagera
  • ***Maxime atamba kutowahofia, awaambia wasitarajie mteremko...

SAFARI ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu inatarajia kuendelea kwa Kagera Sugar kuwakaribisha Yanga kutoka jijini Dar es Salaam katika mchezo utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, picha na mtandao

Katika mechi hiyo ya kiporo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amepanga kumwanzisha golikika kijana, Ramadhani Kabwili baada ya kukosekana kwa Benno Kakolanya huku Kindoki akionekana kushindwa kumudu mashambulizi.

Kabwili aliingia kipindi cha pili katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui FC ambao Yanga waliibuka na ushindi wa magoli 2-1.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zahera, alisema kuwa amejipanga vyema kuhakikisha anatimiza malengo yake ya kuvuna pointi sita kwenye michezo mwili ya Kanda ya Ziwa.

"Nashukuru tumefanikiwa kupata ushindi katika mchezo wa kwanza kule Shinyanga, japo haukuwa mchezo mwepesi, tumejipanga kwa ajili ya kushinda pia dhidi ya Kagera ingawa kuna mchezaji kama Gadiel (Michael) ambaye ameumia, tutamkosa," alisema Zahera.

Kocha huyo aliongeza kuwa ana uhakikia wachezaji wake watafanya kile walichokifanya katika mchezo uliopita na kuendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwania ubingwa wa ligi ambao unashikiliwa na watani zao, Simba.

"Kutakuwa na mabadililo kidogo ambayo siwezi kusema, nataka tufikie malengo yetu ya kuvuna pointi sita huku ugenini, najua si kazi rahisi, tumejiandaa kwa changamoto zote," Zahera aliongeza.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, alisema Yanga wasitarajie mteremko katika mchezo wa leo kwa sababu nao wamejipanga kuondoka na ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.

"Tumejiandaa, kama mwalimu nasema kila kitu kipo sawa, tunasubiri tu mchezo, Yanga ni timu nzuri na inafanya vyema lakini hatuwaogopi, tumejipanga kufanya vizuri katika uwanja wetu wa nyumbani ili kuwafurahisha mashabiki wetu," alisema Maxime.

Habari Kubwa