Yanga yakwama njia panda

10Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Yanga yakwama njia panda
  • ***Sare dhidi ya Al Ahly imewaweka wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye nafasi ngumu kusonga mbele...

WAWAKILISHI wa Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamejiweka mtegoni kusonga mbele michuano hiyo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.

mchezaji wa yanga, Ngoma akipamna na wachezaji wa Al Ahly

Matokeo hayo yana maana, sasa lazima Yanga washinde mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki mbili zijazo nchini Misri. Katika mechi hiyo iliyojaza watazamaji wengi, Yanga ilishindwa kabisa kupenya ngome ya wapinzani wao, ambao sare hiyo ina nafuu kubwa kuelekea mchezo wa marudiano.

Pamoja na Kocha Luis van der Pluijm kufanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwaingiza Geofrey Mwashiuya na Simon Msuva kuchukua nafasi za Amissi Tambwe na Issoufou, bado jahazi la Yanga lilishindwa kubadilisha matokeo. Iliwachukua wageni dakika 10 kufunga bao la kwanza kupitia kwa Amri Gamal aliyetikisa kamba za Yanga kwa kichwa.

Mshambuliaji huyo aliusindikiza kwenye kamba mpira kwa kichwa baada ya kiki ndogo ya adhabu kutoka kwa Abdallah Said kuruka juu ya ukuta wa mabeki wa Yanga walioshindwa kuondoa hatari hiyo.

Baada ya bao hilo, Yanga walitulia na kuwachukua dakika tisa baadaye kufanya matokeo kuwa 1-1 kwa bao la kujifunga wenyewe Al Ahly kupitia kwa Ahmed Hegazy baada ya gonga tamu iliyofanywa na wachezaji wa Yanga.

Wakati huohuo, Azam FC leo watakuwa wenyeji wa Esperance ya Tunisia katika mechi ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi Dar es Salaam. Mabingwa hao wa Afrika Mashariki, anashuka uwanjani bila kuwa na huduma ya beki wa pembeni, Shomari Kapombe na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao ni wagonjwa.

Kapombe yuko Afrika Kusini anakotibiwa baada ya kupelekwa huko kwa matibabu zaidi, wakati Sure Boy anauguza maumivu ya nyonga. Kocha wa Azam, Stewart Hall alisema wamejipanga vizuri kwenye mchezo huo pamoja na kuwakosa wachezaji hao wawili.

Hall alisema kwenye mchezo huo atatumia mfumo mpya ili kuwadhibiti wapinzani wao wanaotumia mfumo wa 4-2-3-1. “Mfumo huu ni kwa ajili ya kupambana na wapinzani wetu, hivyo nitawatumia walinzi wanne," alisema Hall.

Ni wazi kuwa, Erasto Nyoni na Wazir Salum watacheza pembeni na Ramadhan Singano ataziba nafasi ya Sure Boy,” alisema.

Hall alisema amelenga ushindi kwenye mchezo huo na kudai kuwa atapanga kikosi chenye kitakachoshambulia mfululizo na kujilinda pia.

Habari Kubwa