Yanga yalilia bahati Iringa

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
IRINGA
Nipashe
Yanga yalilia bahati Iringa

LICHA ya kipigo cha bao 1-0 walichokipata kutoka kwa Lipuli ya Iringa, kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, amesema timu yake ilicheza vizuri, lakini walikosa bahati kwenye mchezo huo.

kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila.

Mwandila, alisema walitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini hawakuwa makini kwenye kuzitumia.

"Wenzetu wamepata nafasi wameitumia... sisi tulikuwa na nafasi nyingi kuweza kushinda lakini hatukuzitumia, kwangu naona tulikosa bahati kuweza kupata ushindi," alisema Mwandila ambaye aliachiwa jukumu la kukiongoza kikosi hicho kutoka kwa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera aliyesafiri kwenda kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya DR Congo.

Aidha, alisema kupoteza mchezo huo wa juzi hakujawakatisha tamaa ya kuendelea kufanya vizuri kwenye ligi.

"Bado tuna michezo mingine mbele yetu, tuna mchezo mmoja wa Kombe la FA, tunaenda kujipanga kuweza kufanya vizuri kwenye michezo hiyo ya mbele yetu," alisema Mwandila.

Kipigo hicho cha juzi kinaifanya Yanga sasa kupoteza mechi tatu msimu huu, lakini inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 67 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 59, huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 28. Simba ambayo imecheza michezo 20 inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 51.

Habari Kubwa