Yanga yalipa kisasi, yaing'oa APR

20Mar 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Yanga yalipa kisasi, yaing'oa APR

KAMA ilivyotegemewa na mashabiki wa Yanga, kikosi cha Jangwani jana kilikamilisha safari ndefu ya miaka 20 kulipa kiasi baada kuing'oa mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika APR ya Rwanda kufuatia sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo, yanaipa tiketi Yanga kucheza hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 3-2, wakishinda mchezo wa kwanza ugenini 2-1.

APR iliing'oa Yanga katika hatua kama hiyo miaka 20 iliyopita, iliposhinda 3-0 mjini Kigali kabla ya timu hiyo ya Jeshi la Rwanda kufungwa 1-0 Dar es Salaam.

Iliwachukua APR dakika tatu kubisha hodi lango la Yanga na kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Fiston Nkinzingabo aliyefumua shuti kali akimaliza krosi ya Iranze Jean Claude.

Haikuwachukua Yanga muda mrefu kusawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma.

Ngoma alikwamisha nyavuni bao dakika tatu baada ya robo ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa shuti la kushtukiza la umbali wa mita 30 baada ya kudondoshewa pasi fupi na Thabani Kamusoko.

Hata hivyo, kabla ya bao hilo la Yanga, APR nusura wafanye matokeo kuwa 2-1 kama siyo nahodha wake, Jean Claude Iranzi kushindwa kumtungua kipa wa Yanga, Ally Mustafa 'Barthez' wakati akiwa kwenye nafasi nzuri.

Kipa wa APR, Jean Claude Ndoli lifanya kazi nzuri ya kuuwahi haraka mpira uliopigwa na Kamusoko na kugonga mwamba wa juu na kutua jirani na mstari wa goli na kuinyima Yanga bao la pili. Hadi mapumziko matokeo yalikuwa 1-1.

Yanga: Ally Mustafa 'Barthez', Mbuyu Twite, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Pato Ngonyani, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima. Kwa habari zaidi za mchezo huu, soma gazeti la michezo la Lete Raha leo.

Imeandikwa na Renatha Msungu na Somoe Ng'itu.

Habari Kubwa