Yanga yanogesha ubingwa Mbeya

11May 2016
Joseph Kapinga
Mbeya
Nipashe
Yanga yanogesha ubingwa Mbeya
  • ***Mabingwa hao wa Bara wamekamilisha furaha ya ubingwa kwa ushindi huku straika wake Amissi Tambwe akifikisha mabao 21 msimu huu

MABINGWA Yanga jana walinogesha furaha ya ubingwa wao msimu huu kwa ushindi wa mabao 2-0 katika mechi kali ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Ushindi huo uliwafanya mabingwa hao wafikishe pointi 71 wakati Mbeya City inayofundishwa na Mmalawi Kinnah Phiri ilibakia na pointi zake 33.

Kabla hata ya mechi hiyo, tayari Yanga walishatwaa taji bila kushuka dimbani baada ya wapinzani wao wakubwa, Simba kushindwa kuifunga Mwadui FC ili angalau kuwazuia Wanajangwani kutangaza ubingwa mapema.

Katika mchezo wa jana uliokuwa na ulinzi mkali, mashabiki wa Yanga walikuwa wakicheza ngoma na kuimba muda wote wa mchezo.

Vikundi vya mashabiki wa Yanga kutoka matawi mbalimbali vilikuwa na kazi kubwa ya kunogesha furaha ya ubingwa huo.
Kama kuna mtu alionekana kuwa na furaha, basi ni Kocha Hans van der Pluijm pamoja na kocha wa makipa, Juma Pondamali.

Msafara wa wachezaji wa Yanga uliondoka uwanjani ukisindikizwa na ngoma na kila ya mbwembwe, huku mitaani mashabiki wakipunga mikono kuishangilia timu yao.

Katika mechi hiyo, iliwachukua Yanga dakika 16 tangu filimbi ya kuanza mchezo kupulizwa kutikisa kamba za Mbeya City waliokuwa wakielekeza mashambulizi yao kutoka lango la Kaskazini.

Beki wa kati wa Yanga, Vincent Bossou alitumia urefu wake kuwazidi mabeki wa Mbeya City kuruka juu na kupiga kichwa mpira na kufunga bao ndani ya boksi la hatari akiunganisha kona iliyochongwa na Simon Msuva na kumkuta mfungaji aliyemtungua Juma Kaseja.

Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, ambaye jana alikuwa na wakati mgumu mbele ya mabeki wa Mbeya City waliokuwa wakimwinda kila alipogusa mpira, nusura afanye matokeo kuwa 2-0 kama siyo juhudi na uzoefu wa Kaseja kuucheza mpira wa kichwa uliowapita mabeki wa Mbeya City kufuatia krosi ya Haruna Niyonzima.

Mbeya City walijibu mshambulizi baada ya bao hilo, lakini udhaifu mkubwa wa safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Geofrey Mlawa, Salvatory Nkulula walikosa mipango ya kuipenya ngome ya Yanga.

Yanga ilipata pigo mapema kipindi cha kwanza dakika 10 tangu kuanza mchezo baada ya Mbuyu Twite kulazimika kutolewa nje akiwa kwenye machela baada ya kuumia goti na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Telela.

Kadhalika, Bossou naye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kugongana na mchezaji Joseph Mahundi na kumuumiza kichwani na nafasi yake kuchukuliwa na Kelvin Yondani.

Furaha ya ubingwa wa Yanga ilitimia dakika katika dakika ya 84 baada ya Amiss Tambwe kumtungua Kaseja kwa kuubetua juu mpira likiwa bao lake la 21 msimu huu.

Kabla ya bao hilo, Mbeya City watajilaumu wenyewe kwa kosa nafasi mbili muhimu za kufunga mabao.
Dakika ya 63, Salvatory Nkulula alikosa bao la wazi kwa kupiga shuti kubwa juu ya lango la Yanga akiwa ndani ya boksi la hatari.

Tambwe naye alishindwa kubadilisha matokeo ya mchezo baada ya kukosa bao la wazi alipochelewa kuuwahi mpira uliochezwa na kipa Juma Kaseja aliyefanya kazi ngumu kuzuia hatari nyingi za washambuliaji wa Yanga.
Vikosi vilikuwa:

Mbeya City; Juma Kaseja, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Tumba Lui, Haruna Shamte, Kenny ally, Selemani Mangoma, Ramadhani Chombo 'Redondo'/ Rapahael Alpha (dk 69) , Salvatory Nkulula, Geofrey Mlawa na Joseph Mahundi/ Ditram Nchimbi (dk 79).

Yanga; Ally Mustaph 'Barthez', Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Vicent Bossou, Mbuyu Twite/ Kelvin Yondani, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Deus Kaseke.

Habari Kubwa