Yanga yapania kulipa kisasi Al Ahly

22Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Yanga yapania kulipa kisasi Al Ahly

HANS van der Pluijm, kocha wa Yanga, leo anatarajiwa kuwasilisha programu maalum kwa uongozi wa klabu hiyo kwa ajili mechi yao dhidi ya Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

kikosi cha yanga.

Yanga itamenyana na wababe wao wa kihistoria katika michuano ya Afrika, Al Ahly katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Mabingwa Aprili 9 Uwanja wa Taifa kabla ya timu hizo kurudiana jijini Cairo, Misri siku 10 baadaye.

Na baada ya Ahly kuinyanyasa kwa miaka mingi Yanga katika michuano yote ya Afrika, safari hii timu hiyo ya Jangwani imepania kuvunja mwiko kwa kuhakikisha inalipa kisasi cha mwaka juzi cha kung'olewa kwenye hatua ya matuta na timu hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinaeleza kuwa Pluijm leo atakabidhi programu maalumu kwa Kamati ya Mashindano iliyo chini ya Mwenyekiti Isaac Chanji ambayo itakutana na benchi la ufundi chini ya Mdachi huyo na msaidizi wake, Juma Mwambusi kujadili programu hiyo ya maandalizi.

Lakini tayari programu hiyo inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo ratiba ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA inayoinyima fursa Yanga kuweka kambi nje ya Dar es Salaam, achilia mbali nje ya mipaka ya Tanzania.

Mapema wiki iliyopita, uongozi wa Yanga ulitangaza kuwa timu yake itapiga kambi Ubelgiji kabla ya kuivaa Al Ahly, lakini Machi 31 wana mechi ya Kombe la FA na Aprili 2 wana mechi ya Ligi Kuu, hivyo watalazimika kubaki Dar es Salaam.

Ahly imefuzu hatua hii baada ya kuitoa Recreativo do Libolo ya Angola kwa ushindi wa jumla wa 2-1, iliyoupata Cairo baada ya sare 0-0 Angola, wakati Yanga imeitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 2-1 Kigali na kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2014 katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa mikwaju ya penalti, baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani.

REKODI ZAISHUSHA YANGA
Rekodi zinaonyesha tangu Yanga ianze kupata nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), haijawahi kuitoa timu kutoka kaskazini mwa Afrika.
Katika miaka mitano iliyopita, safari ya Yanga katika michuano hiyo imeonekana kufia Misri, Libya ama Tunisia.

2008 - Al- Akhdar
Mwaka 2008, Yanga ilimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho na mchezo wa kwanza ilipangiwa kucheza na Al- Akhdar ya Libya. Mchezo wa kwanza uliofanyika Libya ulimalizika kwa sare ya 1-1, lakini cha kushangaza Yanga ikafungwa bao 1-0 nyumbani katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

2009- Esperance
Mwaka uliofuata, Yanga ilifanikiwa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ilipangwa kuanza na Esperance ya Tunisia (wapinzani wa Azam kwa sasa). Katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Tunis, ilifungwa mabao 3-0 na katika mchezo wa marudiano ikafungwa tena bao 1-0 na kutolewa kwenye hatua ya awali.

2011-Al Ahly
Mwaka 2011, Yanga akashiriki tena michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kujikuta ikipangwa na National Al Ahly ya Misri na katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Cairo, Yanga ili kula kichapo cha mabao 3-0 kabla ya kutoka sare ya 1-1 Dar es Salaam.

2012- Zamalek
Msimu wa 2012/13, Yanga ilishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho ikipangwa na Zamalek ambao hawakuwa vizuri kiuchumi na hata uwanjani, lakini katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam, timu hiyo ya Jangwani, ililazimishwa sare ya 1-1 kabla ya Yanga kuchapwa 1-0 ugenini na kutolewa kwenye michuano hiyo.

2014- Al Ahly
Mwaka 2014, Yanga licha ya kuanza vizuri kwa kuwatoa Wacomoro, Komorizons kwa jumla ya mabao 12-2 katika hatua ya awali, kikosi cha Pluijm kilipangwa na Al Ahly, kikashinda 1-0 Dar es Salaam lakini matumaini ya kusonga mbele yakakatishwa baada ya kupigwa 1-0 ugenini na kung'olewa katika hatua ya matuta.

2015- Etoile du Sahel
Mwaka jana, Yanga ilichuana na Etoile Sportive du Sahel (ESS) katika hatua ya 16-Bora na ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1, wakitoka sare ya 1-1 Dar es Salaam kabla ya kufungwa 1-0 ugenini.

Habari Kubwa