Yanga yapeta  makundi Caf

22Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
CAIRO, Misri
Nipashe
Yanga yapeta  makundi Caf
  • *** Kikwazo kwao ni Waarabu wa Algeria tu...

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wamepangwa kundi mchekea kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika huku timu inayoonekana kuwa kikwazo kwao ikiwa ni Waarabu wa Algeria, USM Alger.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa Cairo Misri jana, Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, ipo Kundi D pamoja na Rayon Sport ya Rwanda, USM Alger (Algeria) na Gor Mahia ya Kenya.

USM Alger ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Algeria inayoshirikisha timu 16, ikiwa na pointi 43, sita nyuma ya vinara CS Constantine baada ya timu zote kucheza mechi 26, huenda ikawa kikwazo kikubwa kwa Yanga kutokana na timu za Kiarabu kuwa na historia nzuri ya matokeo zinapokutana na timu za Tanzania.

Kundi A, ndilo gumu zaidi katika michuano hiyo, kutokana na kujumuisha mabingwa watatu wa zamani wa Kombe la Shirikisho, ASEC Abidjan ya Ivory Coast, Raja Casablanca (Morocco), AS Vita Club (DR Congo) na Aduana Stars ya Ghana.

Kundi B, linaundwa na Renaissance Berkane ya Morocco, Al Masry (Misri), UCD Songo (Msumbiji) na Al Hilal ya Sudan.

Mabingwa wengine wa zamani wa michuano hiyo, Enyimba ya Nigeria, ambao pia walitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mfululizo mwaka 2003 na 2004, wamepangwa Kundi C sambamba na CARA Brazzaville ya Congo, Djoliba (Mali) na AC Williamsville ya Ivory Coast, ambayo ilianzishwa mwaka 1995 na hivi karibuni ikimtangaza Didier Drogba kuwa miongoni mwa memba wa bodi ya klabu hiyo.

Mechi hizo za makundi zinatarajiwa kuanza kupigwa Jumapili Mei 6, huku raundi inayofuata ikiwa ni Jumatano ya Mei 16, mwaka huu.

Raundi ya nne ya michuano hiyo imepangwa kupigwa kati ya Julai na Agosti, na baada ya hapo timu mbili zitakazoongoza katika kila kundi zitatinga hatua ya robo fainali itakayopigwa Septemba mwaka huu.

Michuano hiyo iliyopo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), ni ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani humu baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo bingwa wa shirikisho huibuka na Dola za Marekani 1,250, 000 ambazo ni zaidi ya Sh. bilioni 2.8 za Tanzania.