Yanga yapewa Biashara FA, Tiboroha atema cheche

11Jan 2019
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yapewa Biashara FA, Tiboroha atema cheche

KIKOSI cha Yanga chini ya kocha Mwinyi Zahera, kimepangiwa kucheza na Biashara United kwenye mzunguko wanne wa michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA) itakayochezwa kati ya Januari 25 na 28.

Mbali na Yanga, Azam wenyewe wamepangiwa kucheza na Pamba FC ya Mwanza huku mabingwa watetezi wa kombe hilo, Mtibwa Sugar wenyewe wakipangiwa kucheza na Majimaji ya Songea.

Katika droo iliyochezeshwa jana jijini Dar es Salaam imeshuhudia wababe wa Simba, Mashujaa FC wenyewe watakuwa nyumbani kuumana na Mbeya City huku Singida United wakiumana na JKT Tanzania.

Michezo mingine katika hatua hiyo itashuhudia Stand United wakiumana ugenini na Rhino Rangers, KMC wakiumana na Pan African, Polisi Tanzania wakiwakaribisha Lipuli FC, Coastal Union itakuwa mgeni wa Kitayosce FC, huku African Lyon ikiumana na Friends Rangers.

Aidha, Mighty Elephant itaumana na Namungo FC, Alliance ya Mwanza itawakaribisha La Familia, Dodoma FC itakuwa nyumbani kuumana na Transit Camp, Cosmopolitan itaumana na Dar City wakati Reha FC itakuwa mwenyeji wa Boma FC.

Wakati huo huo, Kampeni za wagombea wa nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa klabu ya Yanga zimezidi kushika kasi ambapo mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk. Jonas Tiboroha amesema amefarijika kuona umati wa wanachama umejitokeza kwa ajili ya kumsapoti katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo huku akiweka wazi kuwa tatizo ndani ya klabu hiyo sio pesa.

Alisema Yanga ina pesa isipokuwa tatizo ni uongozi madhubuti wa kusimamia masuala ya klabu hiyo.

Alisema kutokana na hilo wanayanga wasifanye makosa katika uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika Jumapili katika ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Alisema ana mambo sita ya kufanyia kazi pindi atakapochaguliwa ikiwa ni pamoja na kuweka mipango endelevu ya mabadiliko katika klabu kutokana na Yanga kuwa na matatizo mengi.

Akitoa ufafanuzi alisema Yanga ina fedha isipokuwa haina viongozi ndio maana inaonekana inasuasua
Tiboroha anawania nafasi hiyo pamoja na Mbaraka Igangula katika uchaguzi huo unaosimamiwa kwa pamoja Shirikisho la soka Tanzania (TFF) na uongozi wa klabu hiyo.

Habari Kubwa