Yanga yarudi ilipodumu

15May 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga yarudi ilipodumu
  • ***Tshishimbi aishusha Simba kileleni Ruvu Shooting ikiikimbiza mchakamchaka huku...

KWA mara nyingine tena Yanga imerejea kileleni mwa Ligi Kuu Bara ilipodumu kwa muda mrefu kabla ya wiki moja iliyopita mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba kukalia kiti hicho kwa muda mfupi.

YANGA.

Simba ilishindwa kuendelea kumiliki uongozi wa ligi hiyo baada ya juzi kulazimishwa sare tasa na Azam FC, hivyo kuondoka na alama moja iliyowawezesha kufikisha pointi 82 baada ya michezo 33.

Hata hivyo, Yanga jana iliibuka na ushindi katika mechi yao ya 36 msimu huu baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0, shukrani sikimwendea mfungaji Papy Tshishimbi aliyeziona nyavu dakika ya 15.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kurejea kileleni mwa ligi hiyo kufuatia kufikisha alama 83 moja mbele ya Simba huku wanyonge wao katika mchezo huo, Ruvu Shooting wakibaki nafasi ya 13 na pointi zao 42.

Yanga sasa imebakiza mechi mbili dhidi ya Azam FC na Mbeya City kabla ya ligi hiyo kumalizika, wakati Simba ambayo kesho itashuka Uwanja wa Uhuru kuikaribisha Mtibwa Sugar, ina jumla ya mechi tano mkononi na ikihitaji kushinda michezo mitatu tu ili kutetea ubingwa wao.

Katika mechi hiyo ya jana, Tshishimbi aliyetumia udhaifu wa mabeki wa Ruvu Shooting dakika ambao walikuwa wamesimama kuweka mtego wa kuotea, akautegua na kuuwahi kabla ya kufumua shuti kali lililomshida kipa Abdallah Rashid na kujaa wavuni. 

Dakika ya tano tu ya mchezo, Ruvu Shooting ilikosa bao la wazi, baada ya Full Maganga kuwatoka mabeki wa Yanga na kupiga mpira uliomshinda kipa Klaus Kindoki, lakini kabla haujavuka mstari wa goli, Kelvin Yondani aliuwahi na kuuokoa.

Haikuwa siku nzuri kwa Heritier Makambo aliyeikosesha Yanga mabao manne ya wazi ambapo kama angekuwa makini angeiwezesha timu yake kuibuka na ushindi mnono.

Dakika ya 30 akiwa yeye na kipa, akipiga shuti lililogonga mwamba na kurejea uwanjani, huku mengine akikosa dakika ya 37 na 40. Kipindi cha pili pia Makambo alikosa bao la wazi, huku Tshishimbi naye akikosa mawili.

Ruvu Shooting, ikicheza bila straika wake tegemeo Said Dilunga, iliwaendesha mchakamchaka Yanga hasa kipindi cha pili, lakini ilishindwa jinsi ya kuutumbukiza mpira wavuni.

Mastraika wao Emmanuel Martin anayechezea kwa mkopo akitokea Yanga na Maganga walikosa umakini jinsi ya kumtungua Kindoki ambaye alikuwa akitema sana mashuti yao.

Habari Kubwa