Yanga yashindwa kuipumulia Simba

23Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Yanga yashindwa kuipumulia Simba
  • ***Mbeya City yafanya maajabu dakika za majeruhi baada ya...

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu, Yanga wameshindwa kupumulia mgongoni mwa Simba kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City katika mechi iliyopigwa Uwanja Kumbukumbu ya  Sokoine jijini Mbeya.

Simba juzi ilipata sare ya kwa mbinde kama hiyo  dhidi ya Lipuli FC, hivyo kutoa nafasi kwa Yanga kama ingeshinda jana kuweza kupunguza wigo wa pointi na kuwa tisa wakati huu timu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani ikiwa na mechi mbili mkononi.

Matokeo hayo sasa yanaifanya Yanga kufikisha pointi 48, huku Simba iliyoko mechi mbili mbele ikiwa na pointi 11 zaidi kileleni mwa ligi hiyo inayojumuisha timu 16.

Hivyo, kama Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, itashinda mechi zake mbili za mkononi, itafikisha pointi 54, tano nyuma ya Simba ambayo nayo inaudhamini mnono kutoka kampuni hiyo.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana Jumapili katika Uwanja wa Taifa kwenye mechi ya mzunguko wa pili baada ya ile ya raundi ya kwanza iliyopigwa dimba la Uhuru kutoka sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo ya jana ambayo Mbeya City ilimiliki mpira kwa asilimia 52 dhidi ya 48 za Yanga, hadi kipindi cha pili kinamalizika hakuna timu iliyoweza kushuhudia lango la mwenzake.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mashambulizi ya nguvu langoni kwa mpinzani wake zikitafuta bao la kuongoza, hata hivyo ilibidi Yanga kusubiri hadi dakika ya 58 kuziona nyavu kupitia kwa Raphael Daudi.

Daudi alitupia bao hilo kufuatia kuunganisha nyavuni kwa shuti kali akiitendea haki pasi ya Juma Abdul aliyoitoa akiwa nje ya 18.Mbeya City iliendelea kuliandama lango la Yanga huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, na haikukata tamaa hadi ilipopata bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi kupitia kwa Iddi Suleiman.

Suleiman aliunganisha nyavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliochongwa kutoka wingi ya kushoto katika dakika ya 92, na kuifanya timu yake kuibuka na pointi moja muhimu. 

Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kufikisha pointi 27 katika mechi 25, ilizocheza hadi sasa na ikiendelea kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi hiyo.