Yanga yashusha vifaa

05Aug 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yashusha vifaa
  • ***Mtupiaji wa hat-trick atua, sasa wageukia wa kimataifa, ‘Sure Boy’ naye atajwa...

HAKUNA kupoa! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Klabu ya Yanga kuendelea kunasa nyota walioonyesha kiwango cha juu msimu uliomalizika wa 2019/20 kwa kuingia nao mikataba kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam msimu ujao.

Yanga ambayo msimu huu uliomalizika imemaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa, Simba, huku ikikosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, tangu kufunguliwa kwa dirisha la usajili imekuwa 'bize' kuimarisha kikosi chake na juzi ikitangaza wachezaji 14 iliyoachana nao.

Na jana uongozi wa klabu hiyo, ulikuwa ukimalizana na winga wa Alliance FC ya Mwanza, David Richard, kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Richard ambaye msimu huu uliomalizika amefunga mabao nane, anatua Yanga akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Alliance iliyoshuka daraja msimu huu kumalizika.

Nyota huyo ambaye aliifungia timu yake ya Alliance hat-trick katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC, wakati wakishinda 4-1, mabao hayo akifunga dakika ya tano, 18 na 83 huku lile la nne likifungwa na Sameer Vicent, anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Yanga katika dirisha hili.

Wachezaji wengine ambao tayari Yanga imewasajili tangu kufunguliwa kwa dirisha hili Agosti Mosi, ni pamoja na mshambuliaji Wazir Junior kutoka Mbao FC, beki wa kati Bakari Mwamnyeto aliyekuwa akikipiga Coastal Union, Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar na Yasin Mustapha wa Polisi Tanzania.

Hata hivyo, chanzo chetu kimedokezwa kuwa kwa sasa Yanga ipo katika mpango wa kumnasa kiungo wa Azam FC, Salim Abubakar 'Sure Boy', ambaye ametajwa kuingia kwenye rada za klabu hiyo.

Juzi Yanga ilitangaza kubaki na wachezaji 15 tu kati ya 29 wa kikosi cha msimu uliopita, hivyo 14 kufunguliwa mlango wa kutokea kwa sababu mbalimbali ikiwamo mikataba yao kumalizika na kutohitaji tena huduma zao na baadhi viwango kushuka, wachezaji hao ni pamoja na nahodha Papy Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wengine ni David Molinga ‘Falcao, ambaye naye anatokea DRC na wazawa Jaffary Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vincent ‘Dante’, Mohamed Banka, Mrisho Ngassa, Ally Mtoni ‘Sonso’, Muharami Issa ‘Marcelo’, Ali Ali, Muivory Coast Yikpe Gislain, Mnyarwanda Patrick Sibomana, Mzambia Erick Kabamba na Raphael Daudi.

Akizungumzia kasi ya mafuriko hayo ya usajili, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema hatua wanazochukua katika kukisuka upya kikosi cha timu hiyo ni kwa sababu ya kiufundi na si mihemko ya mashabiki au wachambuzi wa soka nchini, lakini pia akaahidi sasa wanageukia nyota wapya wakuja na ndege (kutoka nje) kusajiliwa.

Bumbuli alisema baada ya kutangaza majina ya wachezaji walioachwa kumekuwa na maneno mengi ya pembeni yakibeza hatua waliyochukua viongozi huku wakihoji usajili huo unafanywa na nani wakati timu haina kocha, jambo ambalo alidai klabu hiyo ina kamati ya ufundi, lakini pia Mwenyekiti wao, Dk. Mshindo Msolla kitaaluma ni kocha.

"Tupo kwa ajili ya kujenga timu na si kubomoa, hatua ambazo zinachukuliwa na uongozi ni thabiti kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chetu kuelekea msimu mpya, mchezaji ambaye ameachwa ama kubakishwa kikosini zipo sababu za kufanya hivyo, uongozi haufanyi kazi kwa mihemko ingawa tunajua Wanayanga wanataka furaha baada ya kuona tumekosa ubingwa msimu huu," alisema.

Kuhusu Tshishimbi, Bumbuli alisema amefika makubaliano na uongozi huku kila upande ukiridhika kuachana baada ya kushindwa kukubaliana dau.

Habari Kubwa