Yanga yatamba itakata mtu leo

27Feb 2016
Na Waandishi Wetu
Dar
Nipashe
Yanga yatamba itakata mtu leo
  • Timu hiyo ya Jangwani iinayomkosa straika Donald Ngoma, itachuana na Cercle de Joachim jijini Dar es Salaam

WAKATI kikosi chake kikiwakosa nyota muhimu, kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm ametamba kuwa hawana kitu kingine cha kufanya leo kwenye Uwanja wa Taifa zaidi ya kushinda na kuikata Klabu ya Cercle de Joachim katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Wachezaji wa Yanga wakijifua kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam jana kujiandaa kuikabili Cercle de Joachim. Picha: Michael Matemanga.

Katika mechi ya marudiano na timu hiyo ya Ligi Kuu ya Mauritius, Yanga inayohitaji sare ushindi au sare ya aina yoyote kutinga hatua ya kwanza ya michuano hiyo, itawakosa viungo Haruna Niyonzima na Salum Telela kutokana na majeraha pamoja na straika tegemeo Ngoma ambaye amefiwa na mdogo wake.

Na katika kuipa uzito mechi hiyo, Pluijm alikiri jana kuwa hakuna mechi nyepesi na timu ndogo kwenye michuano yoyote ya soka na atashusha 'kikosi cha maana' kusaka ushindi wa pili dhidi ya timu hiyo ambayo haipewi nafasi kubwa ya kusonga mbele.

"Haitakuwa mechi nyepesi, kila timu inataka kufanya vizuri ili kusonga mbele," Pluijm aliwaambia waandishi wa habari. "Tutaingia na kasi ya kushambulia ili kutafuta magoli, sipendi mfumo wa kulinda lango."

Mdachi huyo alisema licha ya kuwakosa Ngoma, Niyonzima na Telela, kikosi chake kina nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na kushinda bao 1-0 katika mechi yao ya kwanza nchini Muaritius wiki juzi.

Ikiwa Yanga wakifanikiwa kusonga mbele, watakutana na timu itakayotinga hatua ya kwanza baada ya mechi ya leo kati ya APR na Mbabane Swallows ya Swaziland zitakzochuana kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali, Rwanda. APR ilishinda 1-0 katika mechi ya kwanza.

Kocha wa Cercle de Joachim, Abdel Ben Kacem, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wamepata mbinu za kuifunga Yanga baada ya kuupitia mkanda wa mchezo wao wa kwanza waliopoteza nyumbani.

"Yanga ni timu kubwa na ina uzoefu ina wachezaji wazuri pia, lakini tumekuja kufuata kutafuta ushindi hapa, tunataka kusonga mbele," alisema raia huyo wa Morocco.

Kikosi cha timu ya Cercle de Joachim kutoka Mauritius kiliwasili nchini juzi jioni tayari kuwavaa Yanga.

Habari Kubwa