Yanga yatangulia robo-fainali FA

25Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yanga yatangulia robo-fainali FA

MABAO ya Paul Nonga na Thaban Kamusoko yalitosha kuipa Yanga ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Mlale na kutinga hatua ya robo-fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.

Ikianza kwa mara ya kwanza na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyekuwa nje ya uwanja tangu Novemba mwaka jana, timu hiyo ya Jangwani ilitanguliwa kufungwa goli na timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), dakika ya 21, Shaaban Mgandila alipomalizia krosi safi ya Edward Songo.

Yanga ambao walishinda 3-0 dhidi ya Friends Rangers katika mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo msimu huu, walitulia na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wao wa usajili wa dirisha dogo, Nonga aliyemalizia pasi ya winga wa kushoto Godfrey Mwashiuya dakika saba kabla ya mapumziko.

Kiungo wa kimataifa aliyesajiliwa Jangwani msimu huu akitokea Zimbabwe, Kamusoko aliihakikishia Yanga ushindi dakika mbili kabla ya saa ya mchezo akiitendea haki krosi murua ya Mwashiuya.

Winga huyo pia alikaribia kufunga goli la tatu la wenyeji katika dakika ya 70, lakini shuti lake la mguu wa kushoto lilipanguliwa vyema na kipa wa timu hiyo ya Ruvuma, Noel Murish aliyewahi kuidakia African Lyon ya Dar es Salaam.
Michuano ya Kombe la FA itaendelea kesho kwa mechi mbili, Ndanda FC watakuwa wenyeji wa JKT Ruvu mjini Mtwara, huku Coastal Union wakiwakaribisha Mtibwa Sugar jijini Tanga.

Keshokutwa, Rhino Rangers watakuwa wageni wa Mwadui FC mkoani Shinyanga, wakati jijini Mbeya Tanzania Prisons watacheza dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine.

Raundi ya nne itahitimishwa Jumapili kwa Simba wakiikabili Singida United kwenye Uwanja wa Taifa, Azam FC watasafiri hadi Kilimanjaro kuivaa Panone FC kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi huku Toto Africans wakicheza dhidi ya Geita Gold jijini Mwanza.