Yondan arejea kuwakabili MO Bejaia

10Aug 2016
The Guardian Reporter
Lete Raha
Yondan arejea kuwakabili MO Bejaia

BEKI tegemeo wa kati wa Yanga, Kevin Yondan, juzi alianza mazoezi na timu yake baada ya kukosekana kwa wiki mbili kutokana na kuwa majeruhi.

Kevin Yondan

Yondan aliumia wiki mbili zilizopita katika mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama nchini Ghana wakati Yanga ikilala 3-1.

Hata hivyo, baada ya kukosa mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Yanga ikilazimisha sare tasa, Yondan alifanya mazoezi kikamilifu na timu yake juzi Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga imecheza mechi tano bila kushinda ikilazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa kirafiki, ikifungwa 1-0 mara mbili, na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria na TP Mazembe Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Medeama SC mjini hapa na baadaye kwenda kufungwa 3-1 na timu hiyo nchini Ghana katika mchezo wa marudiano.

Mara ya mwisho Yanga kushinda ilikuwa ni kwenye Fainali ya Kombe la TFF, ilipoibugiza Azam FC 3-1 Uwanja wa Taifa.
Yanga itahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi Agosti 23, mwaka huu.

Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja ina pointi tano kutokana na sare mbili na ushindi mmoja, wakati Yanga inashika mkia kwa pointi yake moja.

Imeelezwa kuwa majeruhi wengine Yanga ni beki Juma Abdul na mawinga Geoffrey Mwashiuya na Simon Msuva. Juma Abdul anasumbuliwa na Malaria wakati Mwashiuya na Msuva wote wakisumbuliwa na maumivu ya goti.

Habari Kubwa