Yondani kamili kuivaa Simba

24Sep 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yondani kamili kuivaa Simba

WAKATI watani wa jadi, Simba na Yanga wakitarajiwa kushuka dimbani Jumapili kuwania pointi tatu za Ligi Kuu Bara, Kocha Mwinyi Zahera, amesema beki wake kisiki na nahodha wa timu hiyo, Kelvin Yondani atakuwa fiti kuwavaa 'Wekundu wa Msimbazi' hao.

Zahera, amesema anataka wachezaji wake wote wawe fiti kwa ajili ya mchezo huo na Yondani jana usiku alitarajiwa kuikosa mechi dhidi Singida United ili kuzidi kuimarika.

"Nina uhakika Yondani atakuwa fiti...baada ya mchezo wa leo (jana), tutaanza mikakati kuelekea mchezo dhidi ya Simba..., nataka kuona wachezaji wangu wote wanakuwa fiti," alisema Zahera.

Alisema Yondani ni mchezaji muhimu kuwapo kwenye kikosi chake kutokana na uzoefu wake.

Wakati Zahera akisema hivyo, Mratibu wa timu hivyo, Hafidh Saleh, alisema Yondani ataanza mazoezi wakati wowote.

Alisema mbali na Yondani, pia Juma Mahadhi anatarajia kuanza mazoezi wakati wowote.

Katika mechi hiyo ya Jumapili, Simba ndiyo timu mwenyeji.

Habari Kubwa