Yondani, Moris nje Yanga vs Azam FC

24Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yondani, Moris nje Yanga vs Azam FC

BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, amefungiwa kucheza mechi tatu kutokana na kumpiga kiwiko mchezaji wa Kagera Sugar wakati timu hizo mbili zilipokutana kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na vinara hao kupata ushindi wa mabao 3-2.

Kutokana na adhabu hizo, sasa rasmi Yondani ataukosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaochezwa Jumatatu pamoja na mechi ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Lipuli, sawa na Aggrey Moris wa Azam FC ambaye naye amefungiwa mechi tatu kutokana na utovu wa nidhamu.

Moris amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na kitendo chake cha kumpiga mchezaji wa Mbao FC wakati klabu hizo zilipocheza hivi karibuni na Paul Peter wa Azam naye amepata adhabu kama hizo baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Mbeya City.

Aidha, wakati Yondani akikutana na kifungo hicho, timu yake, Yanga ya jijini Dar es Salaam imepigwa faini ya Sh. milioni tatu kutokana na kutumia mlango usiokuwa rasmi kuingia kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona ulioko mkoani Mtwara wakati wakishuka dimbani kuivaa Ndanda FC Aprili 4, mwaka huu.

Mbali na adhabu hiyo, Yanga pia itatakiwa kulipa kiasi cha Sh. 500,000 kutokana na mashabiki wake kuwapiga kwa chupa waamuzi wa mechi hiyo iliyomalizika kwa kugawana pointi.

Taarifa iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi ilieleza kuwa pia Ndanda FC nayo imetozwa faini ya Sh. milioni 1.5 kwa kosa la kutumia mlango usiokuwa rasmi wakati walipoikaribisha Yanga katika mchezo wa ligi.

"Ndanda wametozwa kiasi hicho cha faini kwa sababu ndio mara yao ya kwanza wanatenda kosa hilo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Bodi ya Ligi.

Habari Kubwa