Zahera aitabiria makubwa Simba

28Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Zahera aitabiria makubwa Simba

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa Simba ina nafasi kubwa ya kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukilinganisha na wapinzani wao, Mbabane Swallows kutoka Eswatini zamani Swaziland.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, picha na mtandao

Simba inatarajia kuwakaribisha Mbabane Swallows leo katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, Zahera alisema kuwa Simba ina kikosi imara na kama watakuwa makini watafika mbali kwenye mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

"Tangu mwanzo nilisema Simba ina nafasi kubwa ya kusonga mbele, wana kikosi kizuri na walijiandaa vyema, wana faida ya kupata matokeo mazuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanayoshiriki," alisema Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kocha huyo aliongeza kuwa wawakilishi hao wa Tanzania Bara wamepata 'bahati' ya kupangwa na timu isiyokuwa ngumu hivyo wakitumia vizuri nafasi watakazotengeneza wanaweza kupata ushindi mnono na kujiweka kwenye nafasi ya kusonga mbele.

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wataifuata Mbabane Swallows kwao katika mchezo wa marudiano utakaochezwa kati ya Desemba 4 na 5 mwaka huu.

Habari Kubwa