Zahera ashangaa Kakolanya kuwa chini ya Simba

11Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Zahera ashangaa Kakolanya kuwa chini ya Simba

LICHA ya timu yake kupata ushindi katika mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kwa muda mrefu sasa hana taarifa za kipa wake chaguo la kwanza, Beno Kakolanya alipo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, picha na mtandao

Pia Zahera amesema kuwa ameshangaa kusikia meneja wa Kakolanya ni mmoja wa viongozi wa Simba, klabu ambayo ni wapinzani wao hapa nchini.

Kakolanya amekuwa chini ya uongozi wa Suleiman Haroub, mjumbe mpya katika Bodi ya Wakurugenzi Simba ambaye alikuwa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA).

Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Biashara United kutoka Musoma, Mara, Zahera, alisema ni jambo la kushangaza kwa mchezaji wa Yanga (Kakolanya) kuwa chini ya meneja au wakala ambaye ni kiongozi wa Simba.

Zahera alisema kuwa hali hiyo ni hatari na haiwezi kuleta 'afya' kwa mchezo huo hapa nchini.

"Kiongozi wa Simba anakuwa meneja wa Beno, hii ni hatari, hii inakuwa hatari, wakala wake anakuwa kiongozi wa Simba, aaah! golikipa wetu? Mimi sina habari yake tangu nilipokwenda Congo," alisema kocha huyo baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1.

Kakolanya amekuwa katika mgomo baridi wa kuitumikia klabu hiyo akishinikisha kulipwa madai yake ya mshahara wa miezi mitano, hali inayotafsiriwa kuwa inatokana na shinikizo kutoka kwa kiongozi huyo.

Nafasi ya kipa huyo ambaye aliisaidia vema Yanga katika mechi dhidi ya Simba ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana, inashikiliwa na Claus Kindoki na Ramadhan Kabwili.

Habari Kubwa