Zahera atoa neno la ubingwa Yanga

21Jan 2019
Faustine Feliciane
SHINYANGA
Nipashe
Zahera atoa neno la ubingwa Yanga
  • ***Awataka mashabiki kusubiri kwanza michuano ya SportPesa kisha wataona...

LICHA ya kushindwa kujizuia na kuishia kuangua kilio wakati akihojiwa na Azam TV baada ya kupoteza mechi yake ya kwanza msimu huu, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kipigo hicho dhidi ya Stand United hakijawachanganya na kwamba wataendelea kupambana na mechi zijazo ili kufikia malengo yao.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera

Zahera aliliambia Nipashe jana, kuwa kuna ugumu mkubwa kucheza kwenye viwanja vya mikoani na wachezaji walipambana lakini bahati haikuwa yao.

Alisema anafahamu kwa sasa ligi itasimama kwa baadhi ya timu kwa ajili ya kupisha michuano ya SportPesa na kwamba wataitumia kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo ya Ligi Kuu.

"Haukuwa mchezo mwepesi, wachezaji wangu walipambana, lakini hatukuwa makini kuzitumia nafasi tulizozitengeneza, nawapongeza Stand kwa ushindi," alisema Zahera na kuongeza,

"Kwetu bado mapambano yanaendelea, hatujakatishwa tamaa kupoteza mchezo huu... tutapambana kutimiza lengo letu la kutwaa ubingwa msimu huu," alisema.

 

Awatuliza Mashabiki

Aidha, Zahera aliwataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuendelea kuisapoti na kutokatishwa tamaa na matokeo waliyoyapata juzi.

Alisema kufanya vizuri kwa Yanga kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na sapoti ya mashabiki wa timu hiyo.

Yanga inarejea leo Dar es Salaam tayari kushiriki michuano ya SportPesa inayoanza kesho hapa nchini.

Michuano hiyo itashirikisha timu nane, nne kutoka kila nchi, Tanzania na Kenya, ambapo bingwa mbali na kombe na fedha taslimu, hupata fursa ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu England.

Gor Mahia ndiyo bingwa mtetezi wa michuano hiyo, ambayo imeutwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo.

Habari Kubwa