Zahera atoa Sababu Simba kuiua Yanga

18Feb 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Zahera atoa Sababu Simba kuiua Yanga
  • *** Ni baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 Taifa, afafanua kuwa kilichochangia ni...

YANGA imejikuta ikichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa mahasimu wao, Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa, na kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, hakuwa kimya kwani amefichua sababu ya timu yake kukubali kichapo hicho.

kocha wa yanga Mwinyi Zahera, picha mtandao

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo, Zahera alisema walifungwa mchezo huo kwa sababu Simba walikuwa juu zaidi yao.

Aidha, Zahera alisema mbali na hilo, wachezaji wa Simba mmoja mmoja ni bora zaidi ukilinganisha na wachezaji wake.

"Simba walikuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo huu kuliko sisi..., tulikuja uwanjani tukijua kabisa tunaenda kupambana na timu bora na yenye wachezaji wa kiwango kikubwa kuliko sisi, tumekubali matokeo, lakini niwapongeze wachezaji wangu kwa namna walivyopambana, Simba walikuwa bora zaidi yetu," alisema Zahera.

Alisema hakuna wa kumlaumu kwa matokeo waliyoyapata kwa kuwa kila mchezaji alipambana kwa nguvu zake, lakini juhudi zao ziligoma kwa wapinzani wao.

"Hata mabadiliko ambayo niliyafanya ni ya kiufundi zaidi..., Ajibu alionekana kuchoka na pia nilitaka kushambulia zaidi," alisema Zahera.

Alisema anawapongeza Simba kwa ushindi walioupata na wao wanaenda kujipanga kwa ajili ya mchezo unaofuata.

"Tunapitia kwenye wakati mgumu, wachezaji wangu wanapambana na wanajitahidi sana..., baada ya mchezo huu tunaangalia mchezo unaofuata," alisema.

Kwa matokeo ya juzi ni kama Simba iliyofikisha pointi 39 baada ya mechi 16, ilirekebisha makosa yao kwenye mchezo wao wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Yanga baada ya kubanwa na kutoka suluhu na miamba hiyo ya Jangwani yenye alama 58 kufuatia kucheza jumla ya mechi 24 hadi sasa.

Habari Kubwa