Zahera: Hakuna huruma sasa basi

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zahera: Hakuna huruma sasa basi

MBIO za kuwania ufalme wa soka nchini msimu huu zinatarajiwa kuendelea leo wakati Yanga itakapovaana na Ruvu Shooting kutoka Mlandizi, Pwani, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.

Hata hivyo, Yanga itamkosa beki wake wa kati, Andrew Vincent "Dante" ambaye ana kadi tatu za njano lakini nahodha wake, Ibrahim Ajibu aliyekuwa mgonjwa amerejea kikosini baada ya afya yake kuimarika.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema watashuka uwanjani wakiwa hawana huruma na wapinzani wao kwa sababu wanahitaji kupata pointi zote tatu za mchezo huo.

Zahera alisema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mchezo huo, lakini wanajua hautakuwa mwepesi kutokana na mazingira yaliyopo.

Kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisema ligi yoyote inapoelekea ukingoni ushindani huongezeka huku akiitaja changamoto ya hali ya hewa ya mvua pia itachangia kupunguza ubora wa viwango vya wachezaji.

"Tumejiandaa na mechi kama vile tunavyojiandaa katika mechi nyingine, niseme tu hatuna huruma na timu yoyote iliyoko mbele yetu, tunahitaji kupata ushindi, hakuna jambo lingine," alisema kocha huyo ambaye mechi yake iliyopita alifungwa bao 1-0 na Biashara United.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema hawana hofu wala wasiwasi wowote wa kuwavaa Yanga ambao bado wana nafasi ya kuivua Simba ubingwa endapo itateleza katika michezo yake iliyobakia na wao wakishinda yote.

“Yanga inafungika, walianza kufungwa na Lipuli ambao sisi ni wababe wao, wakafungwa pia na Biashara United, njooni muone tunavyowafundisha kandanda," alitamba kiongozi huyo.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Biashara United dhidi ya Alliance FC, timu zote zikihitaji ushindi ili kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja.

Habari Kubwa