Zahera: Hatuviangalii viporo vya Simba SC

12Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Zahera: Hatuviangalii viporo vya Simba SC

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa kamwe hawavifuatilii viporo vya Simba na wanachofanya wao ni kuhakikisha wanashinda michezo yao yote ili kuweza kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Yanga Jumanne wanacheza mchezo wao wa 20 dhidi ya Mwadui FC na huo utakuwa mchezo wa tano zaidi ya mahasimu wao Simba.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Zahera, alisema amewaambia wachezaji wake wajikite katika michezo yao ili waweze kufanya vizuri na si kufikiri majukumu ya wengine.

“Sisi hatufuatilii michezo ya wengine, kile tunachokifanya ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu, tunataka kuona kila mchezo mbele yetu tunavuna pointi tatu na mwisho wa ligi tuone nafasi yetu ni ipi, lengo letu ni ubingwa tu,” alisema Zahera.

Mpaka sasa Yanga imeiacha Simba kwa pointi 17 na baada ya mchezo wa Jumanne, itasafiri kuelekea Shinyanga kuumana na Stand United.

Baada ya hapo itarejea jijini Dar es Salaam kushiriki mashindano ya Sportpesa Super Cup 2019 yanayotarajiwa kuchezwa kuanzia Januari 22 mwaka huu.

Michuano hiyo inatarajia kushirikisha timu nane, nne kutoka Tanzania (Yanga, Simba, Singida United na Mbao FC) pamoja na mabingwa watetezi Gor Mahia, AFC Leopards, Kariobang Shark na Bandari FC zote kutoka Kenya.

Habari Kubwa