Zahera: Yanga kasi pale pale

15Jan 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Zahera: Yanga kasi pale pale

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa wanaosubiri kuona timu yake inapoteza mchezo watasubiri kwa muda mrefu, kwa sababu wao wamejipanga kuendeleza makali katika kila mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara watakayocheza.

Yanga inatarajia kuikaribisha Mwadui FC kutoka Shinyanga katika mechi ya ligi hiyo, itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mazoezi ya jana asubuhi, Zahera, alisema kuwa amewaandaa wachezaji wake kuendeleza makali yao na ana uhakika wataondoka na pointi tatu katika mchezo huo.

“Siwadharau wapinzani wetu, na wao watataka kushinda ili wapate pointi tatu, lakini tumejiandaa vizuri, tunataka kuendeleza rekodi yetu ya kutopoteza mchezo,” alisema Zahera.

Kocha huyo alisema anafahamu wapo wanaotaka kuona timu yake ikipoteza mchezo, lakini wamejiandaa kikamilifu kuondoka na pointi tatu katika michezo yote ya ligi hiyo ili watimize malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu.

“Tunaongoza ligi na tunataka tuendele kuongoza mpaka mwisho, lengo letu ni kutwaa ubingwa... tunajipanga na tutapambana ndani ya uwanja katika kila mchezo,” Zahera alisema.

Naye Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kikosi cha timu hiyo kinaendelea vizuri na mazoezi huku kukiwa hakuna majeruhi.

Alisema baada ya mchezo wa leo, timu hiyo itaelekea Shinyanga kwa ajili ya mechi nyingine inayofuata dhidi ya Stand United ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani humo.

“Baada ya mchezo na Stand tutarejea hapa (Dar es Salaam) kwa ajili ya michuano ya Sportpesa,” alisema Saleh.

Yanga iko kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza michezo 18 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 40 wakishuka dimbani mara 17 wakati Simba iliyocheza michezo 14 iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33.

Habari Kubwa