Zanaco yaipeleka Yanga shirikisho

19Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Zanaco yaipeleka Yanga shirikisho
  • ***Kuungana na Azam kama ikifuzu Swaziland leo, Msuva ‘apeperusha’ bao baada ya...

BAO moja la ugenini lililofungwa katika mechi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika limeipa nafasi Zanaco ya kuwang'oa Yanga kwenye kinyang’anyiro hicho.

Yanga imeaga michuano hiyo baada ya jana kulazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji Zanaco katika mechi iliyokuwa na upinzani kuanzia dakika ya kwanza mpaka filimbi ya mwisho.

Hata hivyo, Yanga ambayo jana iliwakosa washambuliaji wake wa kimataifa wanaocheza katika kikosi cha kwanza, Mzimbabwe Donald Ngoma na Mrundi Amissi Tambwe sasa itacheza mechi nyingine ya mtoano ili kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo itaungana na Azam FC kama itafanikiwa kuitoa Mbabane Swallows ya Swaziland leo.

Yanga ilionekana kuimarika zaidi katika kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake walishindwa kutumia vyema nafasi kadhaa ambazo walitengeneza.

Dakika ya 73, winga Simon Msuva akiwa ndani ya eneo la 18 huku akiwa ameshafanikiwa kuwatoka mabeki wa Zanaco, alipiga juu na kupoteza nafasi hiyo.

Mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Emmanuel Martin naye alipoteza nafasi nyingine kwa kupiga shuti "fyongo" lililoishia mikononi mwa kipa wa Zanaco.

Yanga ambayo iko chini ya Mzambia George Lwandamina itarejea nchini na kuendelea kuwekeza nguvu katika kutetea ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la FA ambayo wanayashikilia.

Yanga: Deogratius Munishi 'Dida', Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Justine Zulu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Haruna Niyonzima na Geofery Mwashiuya.

Habari Kubwa