Zanzibar Heroes, Amavubi kazi ipo

05Dec 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Zanzibar Heroes, Amavubi kazi ipo

TIMU ya soka ya Zanzibar "Zanzibar Heroes", leo inashuka dimbani kucheza mechi yake ya kwanza kuwania Kombe la Chalenji kwa kuvaana na Rwanda (Amavubi) katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Machakos.

Mechi hiyo inatarajiwa kuanza saa nane mchana na Amavubi watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Kenya katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa Jumapili.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes, Hemed Morocco, alisema kuwa wataingia katika mchezo huo kwa lengo moja la kusaka ushindi na kupitia michuano hiyo wanataka kuitangaza timu yao katika ngazi ya kimataifa.

Morocco alisema kuwa hakuna mechi rahisi katika mashindano hayo na wao wamekwenda kuchuana na si kusindikiza wengine.

"Timu yangu iko vizuri, tumejiandaa kupambana ili tupate ushindi, mechi ya kwanza unapopata pointi tatu unajiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele na kutokuwa na hofu yoyote, nimewaambia wasiogope timu pinzani," alisema Morocco.

Alisema wanaamini mbali na kuitangaza Zanzibar, pia michuano hiyo inatoa nafasi ya wachezaji kutangaza vipaji vyao na kupata klabu za nje.

Mechi nyingine ya mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), itakayochezwa leo ni kati ya Kenya (Harambee Stars) dhidi ya Libya ambayo ilitoka suluhu na timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars).