ZFA wajadili changamoto vipaji shuleni

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe Jumapili
ZFA wajadili changamoto vipaji shuleni

MWENYEKITI wa Kamati ya Maridhiyano ya ZFA Taifa, Mwalimu Ali Mwalimu, amesema ipo haja wizara ya michezo kushirikiana na wizara ya elimu katika kuhakikisha Zanzibar inapata wachezaji wazuri kuanzia kipindi wakiwa shuleni.

CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU ZANZIBAR

Ushauri huo ameotua akiwa Rahaleo mjini hapa alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi, aliyokutana nayo kutaka kujua changamoto na mafanikio yalipo katika Kamati ya ZFA.

Alisema kuweka utaratibu wa kuwapo kwa viwanja vya michezo ndani ya shule ni moja ya sharti la lazima la mtu anayetaka kuanzisha shule ili kuendelea na kukuza soka la Zanzibar kuanzia ngazi za chini.

Mwalimu alisema kuwapo kwa viwanja hivyo hususan vile vya mchezo wa soka shuleni kutasaidia kuinua soka la Zanzibar kuanzia ngazi ya chini na pia itasaidia hata pale tunapotafuta timu ya Taifa ya vijana wenye umri sahihi.

Aidha, alisema katika kamati yao kumekuwapo na changamoto, lakini kubwa zimo katika soka ambapo inayoongoza ni uhaba wa viwanja, huku kwa upande wa shule ukichangiwa na vilivyokuwapo kutumika kwa ajili ya upanuzi wa madarasa.

“Hatuna viwanja vya michezo, vipo lakini vichache na  wachezaji ni wengi, na hatuwezi kuwa na wachezaji wazuri kama hatuna viwanja vya kutosha, na hii program ya kuwa na viwanja shuleni itasaidia pia kupata wachezaji wazuri wenye umri mdogo na kuendelezwa vema,” alisema.

Habari Kubwa