ZFF yakumbusha msisitizo corona

26Mar 2020
Hawa Abdallah
Dar es Salaam
Nipashe
ZFF yakumbusha msisitizo corona

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF), limewataka wachezaji, viongozi, mashabiki na wadau wa mchezo huo visiwani humo kutoa kauli na machapisho mbalimbali juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona (COVID 19).

Katibu Mkuu wa ZFF, Mohamed Ali Hilali, alisema jana ugonjwa huo ni janga la kimataifa na kamwe haupaswi kudharauliwa kama baadhi ya wananchi wanavyofanya.

Hilali alisema ZFF inaendelea kuungana na serikali kwa kuzifanyia kazi kauli na maagizo yote yanayotolewa na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed katika kupambana na janga la hilo na corona.

Alisema ZFF inashangazwa kuona baadhi ya watu na taasisi bado zinaendelea kucheza mpira kwa namna ya kushindana (mechi za kirafiki na mashindano yasio rasmi) katika maeneo ya Unguja na Pemba mashambani wakiamini huko hakuna maambukizi.

“Ndugu wanasoka, niwaombe tutekeleze kwa vitendo maagizo na maelekezo tunayoyapata kutoka serikalini na kwa watu tuliowapa dhamana ya masuala ya afya, tusichukulie masihara na wala kuleta dharau katika suala hili... naomba tuendelee kufuata maagizo katika kipindi hiki ambacho dunia inahangaika na ugongwa wa corona," Hilali alisema.

Habari Kubwa