ZFF yamfungia nyota Mafunzo mechi saba

15May 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
ZFF yamfungia nyota Mafunzo mechi saba

KAMATI ya Kusimamia Mashindano na Ligi ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), imemfungia mchezaji wa timu ya soka ya Mafunzo, Mohammed Shaibu Haji, kutocheza mechi saba mfululizo pindi msimu ujao wa 2019/20 utakapofunguliwa.

Mchezaji huyo ambaye klabu yake inashiriki Ligi Kuu Zanzibar, amefikwa na balaa hilo kufuatia kudaiwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hussein Ahamada aliliambia gazeti hili juzi kuwa mchezaji huyo siku mechi ya kufunga msimu wakati wakicheza dhidi ya Malindi alidaiwa kumpiga kiwiko mwamuzi wa kati, Mbaraka Haule aliyekuwa akichezesha mchezo huo kwa madai ya kutotendewa haki.

Hussein alisema adhabu ya mchezaji huyo imetolewa chini ya Kifungu cha 31 cha Kanuni ya kuendeshea mashindano na ligi ambacho kinazungumzia masuala ya nidhamu.

Aidha, alifafanua kwamba mchezaji huyo ataanza kutumikia adhabu yake hiyo mara tu baada ya kuanza kwa msimu ujao.

Habari Kubwa