ZFF yatoa mgao wa fedha kwa timu

30Jun 2020
Hawa Abdallah
Zanzibar
Nipashe
ZFF yatoa mgao wa fedha kwa timu

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar, ZFF, limetoa mchanganuo wa fedha shilingi milioni 21 zilizotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Fedha hizo lengo lake ni kuzisaidia timu za Ligi Kuu ya Zanzibar wakati huu zinarudi kwenye ligi.

Akizungumza na gazeti hili Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFF, Hussein Ahamada Vuai, amesema kila timu ya Ligi Kuu imepewa shilingi milioni moja kwa ajili ya maandalizi ya timu.

Alisema mbali na fedha hizo ambazo klabu zimesaidiwa, lakini pia zimepewa nauli kwa timu ambazo zinaenda kucheza kutoka kituo kimoja kwenda kingine (Unguja na Pemba), pamoja na sehemu ya chakula kwa timu ambazo zitakaa kituo kimoja kwa muda mrefu.

“Hapa itakuwa kwa timu wageni, kwa mfano timu ya kituo cha Pemba itakapokuja katika kituo cha Unguja, serikali watatoa chakula kwa kipindi ambacho watakuwapo hapo, na timu ya kituo cha Unguja itapokwenda Pemba itakuwa hivyo hivyo,” alisema Vuai.

Aidha, alisema hadi sasa ratiba ya ligi hiyo haijibadilika na inatarajiwa kuanza Julai Mosi kama ilivyopangwa na shirikisho hilo kupitia Kamati ya Mashindano na Bodi ya Ligi.

Hata hivyo, ameendelea kuzisisitiza klabu kufuata miongozo yote inayotolewa na Wizara ya Afya katika kujikinga na virusi vya corona.

Habari Kubwa