Zidane awania kuweka rekodi Real Madrid leo

17Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
ROMA, Italia
Nipashe
Zidane awania kuweka rekodi Real Madrid leo

ZINEDINE Zidane leo anaanza safari ya kuandika historia mpya kama Kocha wa Real Madrid atakapooiva Roma itayokuwa nyumbani katika mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya mtoano.

ZINEDINE Zidane

Tangu achukue mikoba ya Rafa Benitez, Zidane amekuwa na mwanzo mzuri kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, akipoteza pointi mbili katika mechi sita za Ligi Kuu Hispania (La Liga).

Kuondolewa kwa timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Copa del Rey na kuwa kwao nyuma kwa pointi nne kwenye msimamo wa ligi dhidi ya Barcelona, kunawafanya kuwekeza nguvu nyingi kwenye michuano hiyo ya Ulaya.

Hata hivyo, Zidane hatakuwa na beki Pepe (mguu) na Gareth Bale anayesumbulia na ugoko, lakini Marcelo amepata nafuu ya bega na atakuwa uwanjani.

Kwa upande wa Roma, watakuwa na wazoefu wawili, Francesco Totti na Daniele De Rossi nao watashuka dimbani baada ya kupata nafuu.

De Rossi na Totti wote walicheza wakati timu hizo zilipokutana katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2008 na kushinda kwa jumla ya mabao 4-2.