Zlatko: Gari limewaka Yanga

16Sep 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Zlatko: Gari limewaka Yanga
  • ***Kikosi chake kitaanza safari ya kuelekea Bukoba kesho, huku akitamba kucheza soka la...

USHINDI ndio jambo pekee ambalo Kocha Mkuu wa Yanga, Mserbia Zlatko Krmpotic, analifikiria kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba, imeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zlatko alisema kikosi chake kipo tayari kwenda kupambana katika mchezo huo na mingine ya ugenini kwa sababu wanahitaji kupata pointi tatu kwenye kila mechi.

Zlatko alisema licha ya kupata ushindi katika mechi iliyopita, anayafanyia kazi mapungufu ya kikosi chake na anaimani ya kufanya vizuri katika michezo yao ijayo ikiwamo dhidi ya Kagera Sugar.

Kocha huyo alisema anahitaji timu yake kucheza soka la kiwango cha juu na ili kufikia huko, kila mchezaji anatakiwa kuonyesha uwezo wake halisi baada ya kukamilisha programu maalumu za mazoezi alizotoa.

Alisema kwa muda mfupi alikuwa nao amebaini wachezaji wake wanahitaji mazoezi kujijenga ambayo yatawaimarisha na kuwasaidia kuingia kwa haraka katika mfumo wake ambao utawafanya wapate matokeo mazuri katika mechi zinazofuata.

“Bado timu haijacheza vile ninavyotaka, ila wachezaji wangu wanapambana na kujitoa, nina imani kila siku zinavyozidi kwenda, kikosi kitakuwa imara, sasa akili yetu inajiandaa na mechi ijayo, tutahakikisha pia tunapata alama zote tatu muhimu katika mchezo huo,” alisema Zlatko.

Alisema tayari ameshawafahamu wapinzani wao Kagera Sugar baada ya kupata taarifa zao kutoka kwa wasaidizi wake ambao wamekuwa karibu wakisaidia kutelekeza majukumu yake vizuri.

"Nimepata taarifa zote kuhusu Kagera Sugar, kupitia taarifa hiyo, nimeshaandaa mbinu na mifumo tofauti ambayo inaweza kutumia kwenye mechi hiyo, nimewajua na tutajipanga kuwakabili," Zlatko alisema.

Naye meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema katika kukijenga vema kikosi chao kuelekea mchezo huo wa kwanza wa ugenini, leo usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini, Dar es Salaam, walitarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege kutoka Zanzibar.

"Tutacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege, hii itampa mwanga wa kuona maelekezo yake aliyowapa wachezaji mazoezini walivyoyafanyia kazi, itamsaidia kiufundi kubaini mahali walipoimarika na idara inayohitaji kuboreshwa," alisema meneja huyo.

Alisema wanatarajia kuondoka jijini kesho na kuelekea Bukoba huku wachezaji wao wakiwa 'fiti' kwenda kupambana kusaka ushindi dhidi ya Kagera Sugar ambayo pia imekuwa ikiwasumbua kila wanapokutana.

Yanga inakutana na Kagera Sugar ambao wametoka kulazimisha sare ya bila kufungana na Gwambina FC kwenye Uwanja wa Gwambina Complex wakati wao wanakumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

Habari Kubwa