Morocco: Viongozi Simba hawajatulia

20Jan 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Morocco: Viongozi Simba hawajatulia

KOCHA Msaidizi wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Morocco, amerejea kwa Zanzibar baada ya kushindwa kufikia makubaliano uongozi wa Simba kukinoa kikosi chao.

WACHEZAJI WA SIMBA

Morocco alitua jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kwa ajili ya mazungumzo ya mara ya pili na uongozi wa timu hiyo, lakini jana alilazimika kurejea Unguja kuendelea na shughuli zake.
Kocha huyo aliiambia Nipashe jana kuwa amewaachia viongozi wa timu hiyo kufanyia kazi mapendekezo yake na wakiafiki, atarejea na kuanza ajira yake mpya ya ukurugenzi wa ufundi kwenye klabu hiyo iliyoanzishwa 1935.
"Kuna mambo hayakwenda sawa na tayari nimesharudi kwetu, viongozi hawajajipanga, bado hawajatulia," alisema kocha huyo ambaye pia ni kocha mkuu wa Mafunzo FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar.
"Niliamua kuondoka baada ya kuona kuna mambo hayakuwa sawa na tulivyokubaliana," aliongeza kocha huyo wa zamani wa Coastal Union.
Hata hivyo, taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya uongozi wa klabu ya Simba, zinaeleza kuwa Morocco alikataa kusaini mkataba baada ya kugundua kiasi cha mshahara walichokubaliana ni tofauti na kile kilichoandikwa kwenye mkataba.
Awali Simba ilitaka kumwajiri Morocco kama kocha mkuu kutokana na kumtimua Muingereza Dylan Kerr, lakini Mzanzibar huyo aliikataa nafasi hiyo na kukubali kujiunga na Wekundu wa Msimbazi akiwa Mkurugenzi wa Ufundi.

Habari Kubwa