Msuva amjibu Kiiza, Yanga ikitakata Dar

25Jan 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
Msuva amjibu Kiiza, Yanga ikitakata Dar

Simon Msuva ndiye aliyefunga goli la kwanza la Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu waliposhinda 2-0 dhidi ya Coastal Unioni Septmba 13 na jana akamjibu Mganda Hamis Kiiza wa Simba kwa kufunga goli la kwanza la timu yake walipoichapa Friends Rangers mabao 3-0 katika mechi yao ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa Taifa.

Simon Msuva.

Kiiza ambaye pia alifunga goli la kwanza la Simba katika ligi ya Bara msimu huu waliposhinda 1-0 dhidi ya African Sports jijini Tanga Septemba 12, alitupia mara mbili wakati Wanamsimbazi walipoibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burkinafaso mjini Morogoro juzi.

Ushindi wa jana umeipeleka Yanga raundi ya nne ya michuano hiyo ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

Msuva, Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa ligi ya Bara msimu ulioita, alimjibu Kiiza kwa kufungua karamu ya mabao ya timu yake alipotikisa nyavu kwa kichwa dakika ya tano baada ya kipenga cha kwanza akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Issoufou Abubakar.

Mchezaji huyo wa zamani wa Azam FC na Moro United alirejea tena nyavuni kwa shuti kali la mguu wa kulia akiwa nje ya boski akimalizia kazi murua ya mshambuliaji wa usajili wa dirisha dogo, Paul Nonga.

Kiiza pia alifunga mabao mawili katika mechi yao ya juzi dhidi ya Burkinafaso juzi.

Straika ambaye amekuwa akisugua benchi la Yanga tangu asajiliwe msimu huu akitokea KMKM, Matheo Anthony, alitupia goli la tatu la Yanga akimalizia kwa kichwa krosi murua ya kiungo Salum Telela.

STAND 0-1 MWADUI
Baada ya kulala 2-0 katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Bara msimu huu, Stand United iliendelea kuwa kibonde wa Mwadui FC baada ya jana kufungwa 1-0 na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

Vikosi vilikuwa:
Yanga: Deogratius Munishi 'Dida', Salum Telela, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva/ Deus Kaseke (dk 64), Haruna Niyonzima, Paul Nonga, Matheo Anthony na Issoufour Abubakar/ Goefrey Mwashiuya (dk 64).
Friends Rangers:

Alphonce Raphael, Twalib Athumani, Mtoro Hamisi, Boniface Nyagawa, Samwel Mathayo, Abbas Wayne, Ally Hamisi, Isihaka Hamisi, Good Hamisi, Eleciter Mpepo na Fred Cosmas.

Imeandikwa na Faustine Feliciane na Renatha Msungu