Mtifuano mkali uchaguzi TFF

12Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mtifuano mkali uchaguzi TFF
  • ***Tisa wamvaa Karia, Hawa awa mwanamke pekee kutaka kumng'oa, Wakili Kibamba afunguka katiba...

ZIKIWA zimebaki saa chache kabla ya dirisha la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uongozi wa juu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kufungwa leo saa 10:00 alasiri, mtifuano huo umezidi kuwa mgumu baada ya jumla ya wagombea tisa kujitokeza kuchukua fomu wakiwa na lengo la kukitaka kiti cha Urais.

Jana waliongezeka wagombea watatu waliochukua fomu za kuwania kiti cha urais wa shirikisho hilo katika Ofisi za TFF na kufanya jumla sasa kuwa 10 pamoja na Karia, ambao ni mwandishi, mchambuzi na wakala wa wachezaji, Ally Saleh kutoka Zanzibar, Rahim Kangezi na mwanadada pekee, Hawa Mniga.

Hivyo sasa wanaungana na Mwenyekiti wa zamani wa Yanga na Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba, kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay Tembele, Deogratius Mutungi, Evans G. Mgeusa, mwandishi na mchambuzi wa soka, Oscar Oscar na Mbunge wa Jimbo la Mwera mjini Zanzibar, Zahor Mohammed Haji.

Kwa upande wa nafasi ya Kamati ya Utendaji kwa Kanda namba 1- Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara na Pwani waliochukua fomu ni wagombea nane ambao ni Lameck Nyambaya, Liston Katabazi, Michael Petro, Saady Mohamed Kimji, Athuman Kingome Kambi, Elyson Mweladzi, Michael Petro na Muharam Mazoka.

Kanda namba 2- Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga ni Khalid Abdallah na Zakayo Mjema huku Abousufian Sillia, James Mhagama na Joseph Ngunangwa wakichukua fomu kwa Kanda namba 3- Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songea. 

Kwa upande wa Kanda namba 4 - Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida waliojitokeza kuchukua fomu ni Mohamed Aden, Osuri Kosuri na Hamisi Juma Kitilia wakati Kanda namba 5- Geita, Kagera na Mwanza ni Salum Umande Chama na Vedatus Lufano na kwa Kanda namba 6- Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora ni Blassy M. Kiondo na Issa Mrisho Bukuku.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kibamba, jana alimwambia mwandishi wetu kuwa mwitiko wa wagombea hasa nafasi ya urais ni mzuri, hivyo anatoa wito kwa wanafamilia wenye nia ya kugombea kutumia siku moja iliyobaki (leo) kuchukua na kurejesha fomu hizo.

"Yapo maoni mengi kutoka kwa Watanzania kuhusu mchakato wa uchaguzi unaoendelea hivi sasa. Ushauri wetu kwao ni kuendelea kufuatilia, kwa vile mchakato unaendeshwa kwa kuzingatia miongozo iliyopo ambayo ni Katiba ya TFF pamoja na Kanuni za Uchaguzi wa TFF," alisema.

Kuhusu wagombea waliowaandikia kuomba mwongozo au kuwapa mapendekezo yao kuhusiana na uchaguzi huo, Kibamba alisema wamewapa majibu kwa maandishi.

Alisema mbali ya kuendesha mchakato huo, moja ya majukumu ya kamati hiyo baada ya uchaguzi ni kutoa tathmini nzima na mapendekezo kama yatakuwapo kwa mamlaka zenye nguvu ya kurekebisha katiba, sheria, kanuni pamoja na taratibu.

"Kama taratibu zilivyo, Katiba au Kanuni za uchaguzi haziwezi kufanyiwa marekebisho wakati mchakato unaendelea," alisema Wakili Kibamba.

Habari Kubwa