Mwigulu asimamisha wachinja ng'ombe

02Jan 2016
Nipashe Jumapili
Mwigulu asimamisha wachinja ng'ombe

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba, amewasimamisha kazi, Mkuu wa mnada wa machinjio ya Pugu na watumishi waliokuwa zamu katika machinjio ya Vingunguti kuanzia Desemba 24 mwaka jana mpaka Januari Mosi mwaka huu, kwa kosa la ubadhirifu wa fedha za serikali.

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba,

Aidha, Waziri amewaagiza watumishi waliosimamishwa kazi kufika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo kesho kwa taratibu nyingine zaidi.
“Leo asubuhi nimerejea kwenye machinjio ya Vingunguti kwa ajili ya kutatua kero zinazowakabili watumiaji wa machinjio haya kutokana na ubadhirifu wa kodi ya serikali kwenye mnada wa Pugu na malalamiko kadhaa yanayogusa wananchi, kuanzia leo hawa watumishi wakatafute shughuli ya kufanya,” alisema Nchemba.
Aidha, Nchemba amesitisha utozaji ushuru eneo la mnada wa Pugu, badala yake makusanyo yote ya fedha za serikali yatafanyika kwenye machinjio ya Vingunguti kwa kutumia mashine za kielektroniki.
“Kwa maana hiyo mnada wa Pugu utakuwa unatumika kutoa vibali tu vya mifugo ili kudhibiti ubora wa mifugo inayopaswa kuchinjwa na siyo kutoza ushuru,” alisema.
Pia aliagiza eneo la kuhifadhia nyama lililokuwa limejengwa kwa fedha za wananchi kushirikiana na serikali lifunguliwe kwa ajili ya wananchi kulitumia na kuhifadhia nyama hiyo.
Nchemba pia aliagiza umeme uliokuwa umekatwa eneo hilo, urudishwe mara moja kwa ajili ya kurahisishia shughuli za machinjio.
“Nimeagiza umeme urudishwe leo (jana), hatua za kuboresha miundombinu ya machinjio hayo nimezielekeza kwa Halmashauri ya Ilala ili zifanyiwe kazi haraka na kwa ubora," alisema Nchemba.
Alisema ili kumaliza changamoto zinazoyakabili machinjio hayo na kupata ufumbuzi wa kudumu, Wizara yake itashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Awali Nchemba alifanya ziara ya kushtukiza katika machinjio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam na kukuta ufisadi wa aina yake ambapo kodi ya zaidi ya mifugo 1,107 hutafunwa na wajanja kwa siku.
Nchemba aliwasili kwenye machinjio hayo ghafla usiku wa saa mbili juzi, hali iliyowashangaza wafanyakazi na wateja wa machinjio hayo, kwakuwa hawakutarajia kumwona Waziri muda huo.
Waziri huyo alishuhudia mifugo mbalimbali ikiwemo ng’ombe na mbuzi ikiwa inachinjwa kwenye hali isiyo ya usafi na picha kadhaa zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha baadhi ya mifugo iliyokufa ikiwa bdo kwenye machinjio hayo.
Kwenye taarifa yake katika mtandao mmoja wa kijamii, Nchemba alisema ameshuhudia utafunwaji wa kodi ya serikali katika mnada wa ng’ombe wa Pugu uliofanyika Desemba 26 mwaka jana.
Alisema kibali kilionyesha kuwa ng'ombe 1,150 walilipiwa ushuru wa mifugo kwenye mnada wa Pugu lakini katika machinjio ya Vingunguti kibali hicho kilionyesha waliolipiwa ushuru ni ng'ombe 300 tu.
Kufuatia hali hiyo, Waziri huyo alisema kuwa mtu yeyote mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi anapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kwani hakutakuwa na huruma kwa wanaoihujumu sekta hiyo.
Aidha, Nchemba baada ya kukagua machinjio hayo, alitoa maagizo kwa uongozi na wahusika wote wenye dhamana kukutana haraka ili kujadili changamoto zilizopo na kuzitatua haraka.
“Naagiza wahusika wa machinjio haya kukutana haraka kujadili masula niliyoyakuta, mjadiliane wenyewe namna ya kutatua changamoto na kero zote zilizopo hapa ndani ya siku moja,” alisema Nchemba.
Machinjio hayo hutegemewa kwa ajili ya kitoweo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani kwa uchinjaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo na shughuli hiyo hufanyika usiku kuanzia majira ya saa 4 hadi 10 alfajiri.
Kumekuwa na malalamiko kwamba mifugo, hasa ng’ombe wanaokufa wakati wakisafirishwa kwa mabasi au treni kutoka mikoani imekuwa hawatupwi na badala yake huchukuliwa na baadhi ya wafanyabiashara kwa bei ya chini na kwenda kuuza mitaani.
Moja ya picha zilizoonekana kwenye ziara ya Nchemba zinaonyesha mifugo iliyokufa ikiwa kwenye machinjio hayo huku baadhi ya walioongozana na Waziri wakiziba pua kuonyesha kuwa kuna kitu chenye harufu mbaya.

Habari Kubwa