Ndugai amesema kweli uzazi kuzingatia uchumi

07Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ndugai amesema kweli uzazi kuzingatia uchumi

SUALA la uzazi wa mpango ni ajenda ya dunia, sababu mojawapo ikiwa ni kupunguza mzigo wa umaskini na makali ya maisha kwa familia nyingi.

Ni kweli kwamba vitabu vitakatifu vinapingana na mpango huo, kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha maagizo ya Mungu.

Uzazi wa mpango umekuwa ukisisitizwa na mataifa yaliyoendelea, ingawa hatukubaliani na approach (njia) zote wanazozitumia kwa sababu baadhi zinakiuka maadili, mila, desturi, miiko na utamaduni wetu  kama taifa.

Hata hivyo, kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya uchumi na ugumu wa maisha, tunapaswa kukubali kuzingatia uzazi wa mpango ili familia zipunguziwe nzigo wa changamoto hizo.

Ikumbukwe kuwa ongezeko la idadi ya watu, inasababisha kupungua kwa rasilimali kunakosababishwa na mahitaji kuongezeka.

Kwa mfano, zamani huduma za msingi za jamii kama elimu, afya, maji, chakula zilikuwa zinapatikana kwa urahisi kutokana na serikali kutoa ruzuku, hivyo kuzifanya zitolewe bila malipo.

Kutokana na mazingira ya wakati ule kabla ya serikali kupungukiwa na uwezo huo kutokana na sababu mbalimbali, kubwa yakiwa masharti ya wakubwa wa dunia, lilikuwa jambo la kawaida kwa familia kuzaa idadi yoyote ya watoto bila kuwapo athari.

Hata hivyo, kwa sasa mambo hayo hayawezekani tena kutokana na kila mtu kuubeba msalaba wake mwenyewe, kama mmoja wa wanasiasa wastaafu nchini, mwenye taaluma ya uchumi alivyowahi kueleza miaka kadhaa iliyopita likiwa ni angalizo lake.

Alichokisema mwanasiasa wakati ule hakikuwafurahisha wengi, lakini alikuwa anaona mbele, na ukweli huo unathibitika sasa.

Juzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitoa kauli ambayo ni changamoto kwa Watanzania na inapaswa kuchukuliwa kwa uzito wake kuhusiana na suala hilo, akiwataka Watanzania kuzaa idadi ya watoto kulingana na uchumi wa familia.

Alitoa rai hiyo jijini Dar es Salaam alipofungua mkutano wa siku mbili wa wabunge wa nchi za Afrika na Asia, waliokutana kujadili ukuaji wa maendeleo na idadi ya watu.Alisema taifa linapaswa kuwa na idadi ya watu endelevu ambao wataishi maisha marefu na wenye uchumi mzuri.

Alieleza kuwa Jambo la muhimu ni kuwa idadi ya watoto ilingane na uchumi wa familia au kaya na taifa, na kuwa kuhusu idadi ya watoto mtu azae wangapi, inategemea na uchumi wa familia husika.

 Alifafanua zaidi kuwa suala la uchumi haliwezi kuangaliwa kitaifa, bali linatakiwa kuangalia katika ngazi ya familia ndipo matokeo ya kitaifa yataonekana.

Alisema Bunge litaendelea na jukumu lake la kuishauri serikali kuhusu sera mbalimbali zitakazowezesha watu kuishi miaka mingi na kuwa nchi yenye uchumi imara.

Alichokisema Ndugai ni kwamba familia zijenge utamaduni wa kuzaa watoto kwa kuzingatia uwezo wao kiuchumi ili kumudu mahitaji kama wa kuwasomesha, chakula, huduma za afya na mengineyo bila kutarajia msaada wa mtu mwingine au serikali.

Tunaamini kabisa kwamba kama jamii yetu itabadilika na itaupokea ushauri huu na kuufuata, bila shaka familia zitapunguza kama si kumaliza kabisa utegemezi, ambao ni kichocheo kikubwa cha umaskini.

Itakuwa vizuri ikiwa wanasiasa wengine wataendelea kutoa elimu hii kwa kuwa wana ushawishi mkubwa katika jamii yetu, na wanasilikilizwa na kuaminiwa na wananchi  wengi.

 

 

 

Habari Kubwa