Njia za ufundishaji madarasa ya awali zisitelekeze KKK

14Jan 2016
Nipashe
Njia za ufundishaji madarasa ya awali zisitelekeze KKK

KWANZA kabisa napenda kumpongeza Rais wa Awamu ya Tano, Dk.John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa elimu bure kuanzia madarasa ya awali hadi kidato cha nne.

Kwa hakika,jambo hili limetua mzigo wa karo uliokuwa umewaelemea wazazi wengi hasa wale wenye kipato cha chini ambao wakati mwingine wanashindwa kumudu hata milo mitatu kwa siku.

Pili nampongeza Dk. Magufuli kwa kukataza ufundishaji wa masomo ya ziada(tuition) kama njia ya baadhi ya walimu kujipatia kipato cha ziada.

Kwa hakika, hili litarudisha ufanisi katika ufundishaji kwa vile walimu wataweka nguvu zaidi kwenye kufundisha wanafunzi darasani, badala ya kutumia muda wao mwingine kufikiria namna ya kujiongezea kipato kwa kupitia dhamana waliyonayo.

Pamoja hayo, ningependa kuishauri serikali hasa Wizara ya Elimu kuipitia upya na kuifanyia marekebisho yenye lengo la kuboresha mitaala inayotumika sasa pamoja na njia za ufundishaji kuanzia madarasa ya awali na kuendelea.
Hii inajikita zaidi kumjenga mwanafunzi kujifunza mambo tofauti tofauti kuanzia darasa la awali ili kumpunguzia kuelemewa ugumu wa masomo anapofika madarasa ya juu Mfumo wetu wa elimu jinsi ulivyo sasa mwanafunzi wa darasa la kwanza anasoma masomo matatu tu, ambayo ni kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) na masomo yanaongezeka kadri anavyozidi kupanda madarasa ya elimu Yaani kadri unavyozidi kupanda mlima, ndivyo unavyopata fursa ya kuona mbali zaidi na kupanua mawazo kwa namna hali halisi jalisi ilivyo.

Lakini kumbe mwanafunzi wa awali, ukiacha masomo ya kuhesabu, kuandika na kusoma anaweza pia kusoma sayansi, jiografia na uraia kwa njia ya vitendo itakayomfanya aelewe zaidi .
Kwa umri wa watoto wa awali, masomo kama haya anayasoma kwa kuwekewa kwenye michezo yao kama vile kuwekewa midoli ya mifano ya wanyama wa aina mbalimbali kwenye maeneo anayochezea yanamfanya avutike zaidi na kuwa na kiu ya kujifunza zaidi hivyo kumfanya fahamu mambo mengi yatakayokuwa na manufaa katika maisha yao.

Ubunifu huo unaweza kuwa kwa mfano, kumjengea mfano wa msitu na kuweka midoli ya wanyama waishio misituni kama vile chui, nyoka, simba na wengineo.
Kama hiyo haitoshi, kuweka maji yenye rangi ya bluu kwenye beseni, halafu kuweka midoli ya samaki wa aina mbalimbali ni ammabo ambayo nina hakika kabisa yatavuta hisia za watoto na kuwafanya waelewe kwa urahuisi maabo mengi zaidi
Ni matarajio yangu kuwa,.kwa njia hii mtoto kwa kupitia mchezo anajifunza aina za viumbe hai na maeneo wanayoishi kutokana na ukweli kuwa mtoto anaelewa zaidi kupitia michezo na si vinginevyo.

Wanafunzi hawa, pia wanaweza kujifunza uraia kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na tukio lolote la kitaifa au kimataifa.
Mfano wa hayo ni kama vile tunaposheherekea sherehe za kitaifa ikiwemo Uhuru na Jamhuri, Mei mosi, mwalimu anaweza kuwaelezea wanafunzi kwa ufupi tu au hata kuwasomea hadithi zinazohusiana na tukio hilo halafu anawaongoza kufanya shughuli mbalimbali za kusheherekea tukio hilo.
Kinachotakiwa kufanywa ni kuwaongoza watoto kuchora picha za mwenge wa uhuru,alama za muungano na mambo mengineyo yatakayowafanya wawe na kumbukumbu ya kudumu
Kwa njia hii, mwanafunzi huyu mdogo atajifunza na kuelewa kwa urahisi sana mambo muhimu yanayofanyika kwa mwaka, hata anapofika madarasa ya juu na kujifunza kwa undani, tayari amekuwa na uelewa wa vitu hivi, kwa hiyo masomo yanakuwa rahisi kwao kuyamudu na si vinginevyo.

Wanafunzi hawa wa awali, pia wanaweza kujifunza kiingereza kwa kusoma alfabeti pamoja na mlio wa sauti inayotoa pamoja na kuwekewa alfabeti za plastiki kwenye michezo yao, ili wazione na kuizoea, kuipenda na kurahisisha uelewa wa somo hili, hasa kipengele cha sarufi (grammar) kwenye madarasa ya juu pamoja.na kusomewa hadithi fupi za Kiingereza na Kiswahili ili wazoeshwe kujisomea vitabu.
Hii itawezesha wafikapo sekondari wamudu somo la fasihi, kwani watoto wengi hushindwa kufaulu somo la fasihi kwa vile wanashindwa kusoma na kuvielewa vitabu vya fasihi.

Kwenye somo la jiografia, mwanafunzi wa awali anaweza kujifunza kuchora kwa mikono yao milima mbalimbali na kubandika darasani au hata kupeleka nyumbani, kuwekewa midoli ya vitu mbali mbali vya kijiografia kwenye michezo yao kama kama vile volcano, majangwa na mengineyo. bila hata kujua wanafunzi hawa watajifunza mambo haya taratibu na kulifanya somo hili kuwa rahisi kwenye madarasa ya juu.

Kama hiyo haitoshi, watoto hawa kama watawekewa michezo inayoendana na mazingira ya nyumbani kama vile kutengewa eneo lililojengwa mfano wa nyumba yenye jiko lililowekwa midoli ya vyakula kama vile mahindi, mchele matunda kama vile embe, papai ni kwamba wataigiza kupika ,basi hapa watajifunza vitu mbalimbali ikiwemo majina ya aina mbalimbali ya vyakula na matunda pamoja na kupata taswira ya mapishi ambayo itakaa kichwani mwao na kuwafanya kupenda kufanya shughuli za nyumbani.

Haya ni mambo machache tu kati ya yale ambayo wanafunzi wa awali wanaweza kufundishwa kwa njia rahisi tu ya michezo na vitendo, ambayo yatawarahisishia uelewa wao wa masomo husika katika madarasa ya juu.

Lakini mambo haya, yanahitaji zaidi vitendea kazi kwa vile hufanyika kivitendo zaidi. Hivyo ombi langu jingine kwa serikali kuweka vitendea kazi vya kutosha kwenye elimu ili kurahisisha njia za ufundishaji, hasa kwa wanafunzi wadogo ambao uelewa wao unahitaji elimu ya vitendo zaidi kuliko kushika chaki.
Naamini ushauri na mtazamo wangu ukifanyiwa kazi kwa uhakika, unaweza kuleta mchango wa mabadiliko katika sekta ya elimu hapa nchini.