Serikali yaridhia hatua zilizochukuliwa na IPP Media

16Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Serikali yaridhia hatua zilizochukuliwa na IPP Media

RAIS John Magufuli amepokea radhi aliyoombwa na gazeti la Nipashe Jumapili, taarifa ya Idara ya Habari-Maelezo ya jana ilisema.

RAIS John Magufuli.

Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abasi, alisema: "Mheshimiwa Rais Magufuli amenijulisha, kupitia taarifa hii niwaarifu IPP Media na umma kwa ujumla kuwa amepokea radhi hiyo."

Nipashe iliomba radhi kwa Rais Magufuli jana baada ya chapisho lake la gazeti dada juzi kuwa na habari iliyosomeka "JPM Akerwa Wanaomtaka Adumu Urais Kama Kagame".

Mbali na Rais Magufuli, Nipashe iliomba radhi kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda kama mwathirika mwingine wa habari hiyo.

Aidha, taarifa ya Dk. Abasi ilisema Serikali imepokea rasmi na kuridhia taarifa ya IPP Media kuhusu hatua za ndani ilizochukua kuenzi uwajibikaji baada ya kuchapishwa kwa habari hiyo Jumapili.

Hatua hizo ni kusitisha uchapishaji wa Nipashe Jumapili kwa miezi mitatu na kuomba radhi binafsi kwa Rais Magufuli na Rais Kagame.  

Taarifa iliwakumbusha wamiliki wa vyombo vya habari kuwa tasnia hiyo inapitia kipindi muhimu katika ukuaji wake na mchango wake kwa umma.

Aidha, taarifa iliwakumbusha waandishi wa habari na wahariri kuwa "hakuna ulinzi mkubwa katika uhuru wa habari kama kutekeleza uhuru huo bila kuathiri haki za wengine ikiwamo maslahi mapana ya nchi kitaifa na kimataifa  na kukubali.

Taarifa hiyo pia ilisema serikali inawahakikishia wananchi kuwa itaendelea kuilea tasnia ya habari, ili izidi kushamiri na kuwa bora zaidi katika kufikia lengo la kuwapatia wananchi habari za uhakika na sahihi ili ziwasaidie katika maisha yao ya kila siku. 

  

Habari Kubwa