Nanenane isaidie kukabili mabadiliko ya tabianchi

08Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nanenane isaidie kukabili mabadiliko ya tabianchi

KILA mwaka Agosti 8, ni Maadhimisho ya Nanenane au Siku ya Wakulima ambayo pamoja na wiki nzima ya maonyesho ya Nanenane yanayofanyika kwa kuzunguka kila mkoa, kuna maadhimisho ya kikanda na ya kitaifa.

Tunawapongeza wakulima, wavuvi na wafugaji wanaoshiriki katika siku hiyo kwa moyo mkunjufu tunasema hongera, wakulima wetu wavuvi na wafugaji kwa kuiwezesha Tanzania kuwa na chakula cha kutosha.

Ni wazi kuwa maadhimisho ya Siku ya Nanenane zama hizi yanafanyika katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi yanayotishia maisha.

Hilo hutokea kutokana na ongezeko la joto duniani, uhaba wa maji, vimbunga, mafuriko na ukame wa muda mrefu nayo pia ni mambo yenye taathira inayojitokeza mara kwa mara kipindi hiki.

Mabadiliko hayo na ongezeko la joto huathiri  uzalishaji, ufugaji na uvuvi baharini kwa kuwa maziwa na mito hupungua kina na wakati mwingine vinakauka.

Kila eneo linaathirika. Wavuvi wanalazimika kuwa na mifumo bora ya kuvua  na kujenga mabwawa ya kulisha samaki.

Tena uvuvi wa samaki nao unatakiwa kufanywa na usimamizi wa hali ya juu kwa kutumia nyavu na teknolojia rafiki.

Kwenye kilimo hali ni mbaya zaidi, wakulima wanaambulia hasara kutokana na ukame, lakini pia huumizwa na uwekezaji kutokana na kutumia fedha nyingi kununua pembejeo lakini hakuna tija.

Si hivyo tu wafugaji nao hasa wahamaji wanaotembea na mifugo yao huathiriwa na ukame unaosababisha vifo na hata magonjwa ya mifugo.

Mabadiliko ya tabianchi yameleta changamoto nyingi ndiyo maana tunaomba serikali na wadau kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kujua mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kutokana na changamoto hizi ni wakati ambao serikali na wadau wana wajibu wa kutumia muda mwingi kuwafunza wahusika namna bora za kutumia mbegu zenye ukinzani na ukame, maradhi na zinazozaa sana kwa upande wa wakulima.

Aidha, kwa wafugaji na muhimu pia kufunzwa namna bora ya kutunza wanyama na kuwa na wanyama wanaoweza kuhimili madhara yatokanayo na tabia nchi.

Pia kutafiti vyakula ambavyo vina virutubisho kwa wanyama, mchanganyiko ambao silazima mnyama ale kiasi kingi lakini hata akitumia kidogo anapata afya na lishe bora.

Yote hayo ni katika jitihada za kupunguza matumizi ya nyasi nyingi, maji pamoja na maeneo makubwa ya kulishia vitu ambavyo vina athari kwa dunia ya leo kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mafunzo ya mara kwa mara na kuandaa mbinu za kimkakati kukabiliana na matatizo ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi yatawafanya wakulima, wafugaji na wavuvi kupata mbinu na mikakati mipya ya kuboresha shughuli zao.

Wakulima ndiyo walio kwenye hali mbaya zaidi hivyo Nanenane zitumike kuboresha shughuli zao.

Tunaamini kuwa vituo vya utafiti zama hizi pamoja na kuhimiza mabadiliko kiufugaji ni lazima kuangalia mbinu mbadala za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuleta teknolojia nyepesi na nafuu kwenye kilimo hasa mazao ya mkakati ambayo yanatanufaisha taifa na wakulima kimapato.

Shime serikali na wadau Nanenane za wakati huu zisiwe za maonyesho ya kibiashara zaidi bali zijikite kwenye mbinu na teknolojia mpya zitakazosaidia kukuza na kuongeza uwekezaji kwenye sekta za uvuvi, kilimo na ufugaji.

Habari Kubwa