Waathirika dawa za kulevya wanusuriwe kupitia njia hii

08Aug 2019
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waathirika dawa za kulevya wanusuriwe kupitia njia hii

BAADHI ya wawakilishi wa wananchi bungeni, wamewahi kuibua tuhuma nzito juu ya tabia chafu zinazofanywa na baadhi ya wamiliki wa nyumba za kutibu waathirika na dawa za kulevya, maarufu ‘sober house.’

Ilikuwa Aprili mwaka jana mbunge kijana, Halima Bulembo, alipodai baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo huwachoma tena sindano za dawa za kulevya, vijana wanaokaribia kupona, ili wasitoke ‘sober house.’

Kwa mujibu wa Bulembo, lengo kubwa la kufanya hivyo, ni kutaka kuendelea kuingiza pesa kupitia waathirika na alitaka maelezeo kutoka serikalini, kuhusu hatua zinazochukuliwa.

Baada ya tuhuma hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama, alikiri kuptia kauli sio mara ya kwanza bungeni na akawaonya wahusika wanaoendekeza nyendo hiyo.

Pamoja na hayo, mjadala bado unaendelea. Kwa maoni yangu, kuna haja ya serikali kutafuta ufumbuzi katika hilo kwa kujenga 'sober house' nyingi nchini na itakayowakusanya waathirika wa dawa za kulevya waishi humo.

Hizo zinapaswa kuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji mali, ili waathirika wanapopona, wageuke kuwa wazalishaji mali, zikiwamo za kilimo inayowakwamua kiuchumi.

Nasema hivyo, kutokana na ukweli waathirika walio nje ya ‘sober house’ wakitokea majumbani kwenda kupata matibabu vituoni kisha wanarudia mazingira yao, wanakumbwa na vishawishi vinavyowafanya warudie ‘uteja' hata baadhi hatua mbaya kama vile kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya, mtu anapotumia methadone (dawa za matibabu) na kurudia dawa za kulevya, ana uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha na tena kifo cha ghafla kwa kuzidisha matumizi.

Hivyo, ili kuwanusuru waathirika ni vyema kuwa na sober house nyingi nchini zenye maeneo kwa ajili ya uzalishaji mali na kuwaweka wote huko wakiwa chini ya uangalizi wa hali ya juu.

Ni ukweli usiopingika kwamba matumizi ya dawa za kulevya ni moja ya matatizo makubwa yanayozikumba nchi mbalimbali duniani, ikiwamo Tanzania, vijana wanatajwa kuathirika zaidi kwa dawa hizo.

Madhara ya dawa ya kulevya yako katika nyanja mbalimbali kwani watumiaji wanaweza kushiriki katika vitendo vya kihalifu ikiwamo wizi na ukahaba ili kupata fedha za kununua dawa hizo.

Dawa hizo zinasababisha utegemezi wa kisaikolojia na utegemezi wa kiuchumi. Pia, inafanana na kujichimbia kaburi bila kujua, athari za kiakili na kimwili.

Janga mojawapo la kiafya liko kwa watumiaji, ni kuambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU) kwa mtu sindano kutumiwa na mtu zaidi ya mmoja, hali inayokaribisha maambukizi.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Ukimwi (UNAIDS), ingawa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU), duniani kote yamepungua, lakini maambukizi miongoni mwa wanaojidunga sindano za dawa hizo, hayapungui.

Ripoti iliyonduliwa Machi mwaka huu mjini Geneva, Uswisi, ikionyesha asilimia 99 ya watu wanaojidunga dawa za kulevya wanaishi katika nchi ambazo hazitoi huduma ya kupunguza madhara.

Inafafanua zaidi kuwa katika wastani wa watu milioni 10.4 wanaojidunga sindano za dawa za kulevya mwaka 2016, zaidi ya nusu walikuwa wanaishi na maradhi ya homa ya ini (Hepatitis C) na wanane ambao ni wastani wa nusu orodha hiyo, walikutwa na VVU.

Shirika hilo linashauri kuwaweka watu katika vituo vya malezi, wakihakikishiwa wanapata huduma bora za afya za kijamii kwa misingi ya utu, pasipo na ubaguzi dhidi ya dai la makosa yao na kwamba maisha yanaweza kuokolewa na maambukizi mapya ya VVU kupungua.

Pia iko wazi na sahihi kutambua juhudi zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha matumizi ya dawa za kulevya yanakoma nchini, lengo kuu ni kuokoa nguvukazi ya taifa, ambayo kimsingi ni kundi la vijana.

Nchini, serikali imeanzisha vituo vingi vya kutoa dawa zinasaidia waraibu kuacha matumizi ya dawa za kulevya, pia kuna nyumba za kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya.

Kimsingi, zote ni jitihada za kutaka kuhakikisha watumiaji dawa za kulevya wanaachana nazo na kurejea hali ya kawaida, hatimaye wenye manufaa kwa familia, jamii na taifa lao.

Mtazamo mkubwa niliyo nao kuptia mjadala huu, ni kwamba ushauri ufanyike kitaifa kwa kuanzishwa maeneo ya kutosha ya shughuli za uzalishaji mali, wahusika wapewe faida kwa familia, jamii na taifa lote.

Habari Kubwa