Mrajisi: Huu ndio Ushirika, imesimama ‘damudamu’ na sekta kilimo

09Aug 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mrajisi: Huu ndio Ushirika, imesimama ‘damudamu’ na sekta kilimo
  • Mrajisi: Huu ndio Ushirika, imesimama ‘damudamu’ na sekta kilimo …simulizi za soko, manunuzi, mtaji

JANA ilikuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, maarufu Nanenane. Uchumi wa nchi  kwa kiasi kikubwa uko katika historia ya kushikiliwa na sekta ya kilimo, ambayo katika sura yake ya kufanikiwa, inashirikiana na sekta, vyombo na wadau wengi.

K.N.C.U

Ikiwa ni mwajiri zaidi ya theluthi tatu ya Watanzania, kilimo, chombo cha ushirika kilichotapakaa katika sehemu nyingi nchini, ni mdau wake wa karibu, ikichukua sura ya mtaji, muunganisho na masoko ambako ina nafasi kubwa.

Hapo inapozungumziwa ushirika, imeshikamana kupitia chombo kiitwacho, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Nchini. Hicho ni chombo muhimu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu yake, chini ya uratibu wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini,Tito Haule,

Anasema katika kutekeleza majukumu yake, inaongozwa na Mpango wa Maendeleo Endelevu, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa na miongozo ya kisheria, ikiwamo kilimo .

Haule anasema uhamasishaji uliofanywa na tume pamoja na wadau wengine wa ushirika kwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini, umesababisha kuanzishwa na kusajiliwa vyama vya ushirika 2,377 kuanzia mwaka 2015 hadi Septemba mwaka jana.

Haule anasema ongezeko hilo limefanya jumla ya vyama vyote vya ushirika nchini kufikia 11,149 , Katika mjumuiko huo kuna Shirikisho la Vyama vya Ushirika; vyama vikuu vya ushirika 51; miradi ya pamoja 39; na vyama vya ushirika vya msingi 11,058, ambavyo vyote vina majukumu makubwa ikiwamo kukuza kilimo nchini

Anasema, katika taratibu za uongozi, wajumbe wa bodi wanapaswa kukaa madarakani kwa kipindi cha muda wa miaka mitatu na kufanyika uchaguzi mwingine wa viongozi.

 “Lengo la usimamizi wa chaguzi hizo ni kuhakikisha zinaendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni za vyama vya ushirika vilivyopo.

“Tume imeendelea kutatua migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ukosefu wa elimu juu ya dhana ya ushirika, kutofuata sheria na taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika na ubadhilifu,” anafafanua.

Haule anasema, pia wanashirikiana na Wizara za Kilimo, pia Ofisi ya Rais -Serikali za Mitaa na wadau wengine kuhamasisha Watanzania hususani vijana, wanawake na vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika kujiunga au kuanzisha vyama hivyo vya ushirika.

Anasema tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masoko wakiwamo wa Bodi ya Leseni za Ghala, Soko la Bidhaa, Wakala wa Vipimo na bodi za mazao, zimeendelea kuvijengea vyama vya ushirika uwezo wa masoko ya bidhaa zake.

USHIRIKA NA MKULIMA

Haule anasema matumizi ya mifumo ya masoko, imechangia kuboresha mauzo na kuimarisha ushindani wa mazao ya kimkakati na mengine ya biashara, zikiwamo kakao, ufuta na miwa.

Pia, anasema mfumo wa ununuzi wa mazao ya kilimo unahusisha wakulima kukusanya kupitia vyama vya ushirika vya msingi, wakilenga masoko ya pamoja kwa njia ya minada au uuzaji moja kwa moja.

Aidha, Haule anasema ununuzi wa mazao ya mkulima kupitia vyama hivyo kunasababisha wakulima kuwa na nguvu ya pamoja ili kupata bei zenye tija; kuanzisha na kuendesha maghala na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao.

Haule anaeleza mtazamo mkuu katika kilimo nchini, ni kuhakikisha inamsogezea mkulima vipaumbele vyake.

STAKABADHI GHALANI

Mdau maarufu wa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Michael Tsaxara, anasema ununuzi wa mazao kwa njia ya ushirika ni bora na umelenga kumsaidia mkulima kukaa mbali na urasimu uliokuwapo, hata kumfanya mkulima asinufaike na kilimo chake.

“Ununuzi wa mazao kwa njia ya ushirika mkulima anapata fedha zake zote bila ya kuwapo kwa mtu wa kati, mathalani kwenye ufuta kupitia vyama vya ushirika zao hilo liliuzwa kwa Sh. 3,000 kutoka Sh. 1,800 iliyokuwa awali na wakulima wamepata faida," anasema.

Tsaxara anasema, kumekuwapo faida kubwa ikiwamo kudhibitiwa walanguzi wa mazao wanaopangia bei wenyewe na kutumia vipimo visivyohakikiwa, jambo lisilokubalika katika soko la mazao.

Katika hilo, anatoa mfano kwa kutoa pongezi kwenye msimamo wa Tume ya Taifa ya Ushirika, kutaka zao la dengu linunuliwe kwa njia ya mnada na si wakala au wafanyabiashara kununua kwa wakulima majumbani na mashambani.

 Katika namna ya kujigamba, anasema mbadala umekuwa vyama vya msingi kujikusanya kutafutia masoko kwa pamoja.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani(Corecu), Rajabu Ng'onoma, anaunga mkono kuwa uuzaji mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, umekuwa wa faida kubwa kwao.

Anataja faida hizo kuwa ni kuuza mazao kwa bei kubwa, tofauti na kila mkulima kuuza mazao kwa bei yake binafsi, ambayo wakati mwingine hawapati faida na inageukia kumnyonya mkulima.

USHIRIKA VS MASOKO

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dk. Titus Kamani, anasema wameendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda kupitia vyama vya ushirika na tayari vyama 108 vinamiliki viwanda vidogo na vya kati vipatavyo 166.

Anasema, ni lazima vyama vya ushirika kupitia kwa maofisa wake walioko nchini kote, kutafuta masoko yenye tija kwa manufaa ya wanaushirika kila waliko.

“Tafuteni watu wazuri wa kutafuta masoko mazuri ya mazao ya wana - ushirika na msiwe watazamaji, nawahakikishia mkipata soko zuri la zao, sisi tutatoa idhini mkauze popote.

“Lakini tunataka tuondoke kwenye kuuza mazao ghafi, tuuze mazao yaliyosindikwa ili kulinda ajira kwa watu wetu na kuongeza thamani ya mazao yetu,” anasema Dk. Kamani.

Anasema zaidi kuwa: “Lazima mali za ushirika zirudi, viongozi orodhesheni mali za ushirika zilizo kwenye mikono isiyo sahihi zilizoshindwa kurudishwa, orodha iwasilishwe tume. Mali zote hasa ardhi na majengo zinazomilikiwa na ushirika zitafutiwe hati.”

Suala la ushirika linaenda mbali, kwamba linagusa mitaji midogo na mikubwa, kupitia vyama vya kuweka na kukopa vilivyoshika kasi nchini kote, pia baadhi ya benki na asasi za kifedha, kutoa mikopo kwa mkondo huo.

Pia, ni mtazamo ambao umekuwa na historia ndefu kuwaunganisha wanajamii kiuchumi, kijamii na hata kisiasa, kabla na hata baada ya uhuru wa Tanganyika.

Itakumbukwa, baadhi ya vyama vya ushirika mfano vya Bukoba mkoani Ziwa Magharibi (sasa Kagera) na KNCU ya Kilimanjaro inabeba historia pana, kupita  uchumi na maendeleo kama ya elimu na siasa ya wakazi wake.

Hata katika kipindi kabla na  baada ya uhuru, katika mfumo wa chama kimoja, ushirikika ulikuwa moja ya idara muhimu za vyama tawala wakati huo, Tanu na badaaye CCM.

Hivi sasa inashuhudiwa  ushirika ulivyo mithili ya ‘chanda na pete’na mfumo wa ununuzi katika kilimo nchini na uzalishaji mazao kama kahawa katika ,maendeo kama ya Kagera, Kilimanjaro, Wilaya za Mbiga (Ruvuma) na Mbozi mkoa wa Songwe.

Habari Kubwa